NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Kampuni 26 kutoka shule 11 za sekondari mkoa wa Arusha na Kilimanjaro zimeshiriki katika maonyesho ya kitaifa ya The Faundation for Tomorrow na JA Afrika yaliyolenga kuonyesha mawazo, ujasiliama na ubunifu wa wanafunzi ili kuwezesha upatikanaji wa elimu bora bila kujali asili yao ya kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kumpata mshindi atayenda kuliwakilisha taifa katika maonyesho ya kikanda Afrika yatakayo fanyika nchini Mauritius.
Akifungua maonyesho hayo mkuu wa Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda Yaliyofanyika mkoani Arusha alisema kuwa maonyesho hayo ni ushahidi wa kazi za vijana wa kitanzania kuwa wanao uwezo mkubwa wa kuchangia katika uchumi wa taifa kwa kutumia fursa mbalimbali za kujiajiri au kuajiriwa ambapo wameona kwa vitendo ujuzi na maarifa ya vijana hao.
“Niwapongeze sana
vijana (wanafunzi) ambao mmeshiriki katika maonyesho haya, kwanza kwa kazi kubwa ya ubunifu lakini jinsi ambavyo mmejipanga, nimeona vijana wenye ujasiri mkubwa mnavyojieleza na mshindi ukatuwakilishe vyema huko Mauritius ili tuweze kuonyesha kwamba vijana wa kitanzania mnao uwezo mkubwa na mpo tayari kushinda katika nyanja za kimataifa,” Alisema.
Sambamba na hayo alizisihi shule zote 11 zilizoshiriki katika maonyesho hayo kuendeleza miradi au kampuni ndani ya shule ili kuendelea kuwajengea vijana vipaji na kuwaandaa vema kwaajili ya kukabiliana na matatizo mbalimbali katika ulimwengu wa sasa hasa ukosefu wa ajira.
Alisema kuwa zoezi la kwenda kuzunguka mitaani kutafuta ajira haliendi kutokea kwa vijana hao kwani tayari wana msingi wa kwenda kujitegemea ambapo alisisitiza vijana hao kusaidiwa kwenda kusajili mawazo yao ili yasiweze kuibiwa na kuwafaidisha watu wengine na kuwaacha wao wakiwa hawana kitu
Kwa upande wake Mkurugenzi wa The Faundation for Tomorrow Noah Kayanda alisema kuwa lengo la maonyesho hayo ni kuwezesha kizazi cha sasa na baadae kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha yao kwa kuwapa ujuzi mahiri wa elimu ya kifedha, ujasiliamali, usimamizi wa miradi pamoja na utayari wa kufanya kazi kwa kujiajiri wao wenyewe.
Alieleza kuwa kiini cha programu hiyo ni kukuza ubunifu na uvumbuzi miongoni mwa wanafumzi ambapo kwa kupitia matatizo mbalimbali washirika wanapewa jukumu la kuunda kampuni itakayoleta suluhisho bunifu yenye mikakati ya kiujasiriamali inayozingatia kutunza mazingira kwa dhana ya uchumi wa kijani.
“Katika programu hii tumeweza kuwafikia wanafunzi 500 tukiongozwa na dhima ya Green Inovation inayozingatia kutunza mazingira na inalenga wanafunzi wenye umri wa miaka 12 hadi 22 ili kuweza kulea talanta, matarajio na ndoto za vijana wetu na kama mlivyoona leo tumeshudia mabadiliko kutoka kwa wanafunzi wetu ambao sasa wana ujasiri, ujuzi na umahiri muhimu na wako tayari kukabiliana na kuwajibika kwa jamii zao kwa kutatua changamoto za sasa na hata baadae, ”Alisema.
“Wanafunzi wameonyesha ujuzi mkubwa na usimamizi wa miradi na uvumbuzi ni dhairi kwamba kazi yao inajumuisha mpango anuwai ambayo inashughulikia matatizo ya eneo husika na kuzingatia dhana ya maendeleo endelevu kwani ujuzi huo ni muhimu katika ulimwengu wa leo unaobadilika kwa haraka na ni stadi mzuri za maisha zitakazowasaidia katika maisha ya kila siku,” Alieleza.
kwa upande wao wanafunzi walioshinda katika maonyesho hayo kutoka shule ya Arusha science Baraka Kileo mkurugenzi wa kampuni itwayo Boom Take iliyokuja na Application inayopatikana Play store ambayo inamuwezesha mkulima kuskani na kujua tatizo la mmea, jinsi ya kupata dawa na mengineyo kwa wale wenye simu janja lakini pia mkulima aliye na simu ndogo za kawaida kuweza kuuliza maswali na kujibiwa ambapo alisema kuwa wataenda kuiwakilisha nchi ipasavyo na kuhakikisha ushindi ukurudi Tanzania.
“Tutahakikisha tunajipanga kwa ubora zaidi kwenda kuleta ushindi Mauritius na kuhusu mashindano haya yanatusaidia kwani yametufungua akili ya kwamba tusitegemee tu kupata ajira bali kuangalia matatizo katika jamii na kuja na ufumbuzi ili kusaidia jamii yatu,” Alisema







0 Comments