-ZAMBIA TANZANIA HOI.
-HUDUMA ZAFIFIA.
-TRENI YAKODISHWA.
Na Fredrick Siwale MDTV Media . fredericksiwale71@gmail.com
TAZARA Mfupa ngumu kwa Serikali na lisipofuatiliwa kwa umakini Shirika hilo linaloendeshwa kwa Ushirikiano wa Nchi mbili za Tanzania na Zambia linakwenda kufa kifo cha mende kama yalivyokufa Mashirika mengine ya Umma.
Uchunguzi umebainisha kwamba kwa sasa TAZARA linadaiwa kuendeshwa kwa hasara ili hali kuna baadhi ya Watu wananeemeka, haiingii akilini kuwa TAZARA inakwenda kufa kifo cha kibaya kama Mashirika ya Umma mengine yalivyo kufa.
Binafsi katika uchunguzi wangu hainiingii akilini kuwa TAZARA inakwenda kufa ,bali nina amini kuwa ndani ya Shirika hilo kuna mchwa unalitafuna kwa kasi kwa baadhi kujinufaisha wenyewe ili hali Serikali haijui kinachoendelea .
TAZARA ni Shirika la reli ya Uhuru inayoendeshwa kwa Ushirikiano na Mataifa ya Nchi mbili za Tanzania na Zambia , reli hii ya Uhuru ilijengwa mwaka 1974 kwa kulipa gharama za Ujenzi kwa ufadhili wa Nchi ya China bila kuwepo hiki tunacho kishuhudia sasa cha utengano.
Uchunguzi umefanyika kwa kina na kubaini kuwepo kwa mgawanyiko ndani ya taasisi hii ya kujivunia baada ya kubaini kuwa treni ya Zambia ya Express imesitisha safari zake kati ya Tanzania na Zambia kufuatia kinachosadikika kuwa ni kushindwa kutoa huduma nje ya mipaka ya Nchi hiyo ya Zambia kwa kuwa linajiendesha kwa hasara.
Katika uchunguzi wake Matukio daima APP iligundua kuwa Treni ya kutoka Nchini Zambia ijulikayo kwa jina la Mukuba inatoka Kapiri Mposhi na kuishia Nakonde kwa upande wa Zambia na kuwaacha abiria na Wageni wengine kubakia wakihamgaika.
Sakananji Simchimba akiwa Tunduma alisema kuwa ndani ya Shirika Kuna ombwe kubwa la Wababaishaji na walajiji ambao hawaifahamu kesho yao iwapo TAZARA itakufa.
Shirika limegawanyika Zambia kivyao na Tanzania kivyao treni ya Tanzania ya Kilimanjaro ikitokea Dar es salaam inaishia Mbeya na kurudi
sababu zikitajwa kuwa ni ukata ukata wa kiuchumi ndilo tatizo kuu.
Samsoni Anyelwisye kwa upande wake alisema TAZARA inafanyiwa hujuma na Watu maana treni manehewa yanajaa iweje kuwepo na hasara ili hali treni inabeba abiria na inajaza kama hakuna wizi na udokozi wa fedha za Umma unaofanyika ? Alihoji Anyelwisye.
Sababu za Wazambia hao kujitenga kutoa huduma inadaiwa ni ugumu wa uendeshaji kwa TAZARA upande wa Tanzania kwani treni ya Mukuba inaweza kujiendesha kwa faida kidogo kwa safari ya Kapiri Mposhi hadi Nakonde kwenda na kurudi kuliko kufika hadi Dar es salaam ambako inaendeshwa kwa hasara .
Serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka kuinusuru TAZARA, kwani treni ya Tanzania kutoka Dar es salaam hadi Mbeya na kurudi sio lengo la abiria bali ilitakiwa kuendelea na safari hadi Zambia kama ilivyokuwa awali.
Kuliacha Shirika hilo kufa ni kupoteza moja kati ya tunu ambazo Taifa la Tanzania iliachiwa na Waasisi Wawili wa Tanzania na Zambia Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Dr.Keneth Kaunda wa Zambia .
Kwa sasa treni ya Zambia Mukuba inajikongoja ili hali treni ya Tanzania ya Kilimanjaro ya Dar es salaam Mbeya ikiwa hoi bin taabani ikiwa imepoteza muelekeo wake wa ratiba kwa kuwepo au kutokuwepo, sio ajabu treni kushindwa kupandisha kilima na kuanza kurudi nyuma au kwenda mbele huku ikikosa breki na kuhatarisha maisha ya abiria.
"HII IMEUZWA AU MALI YA UMMA "
Uchunguzi wa kina uliofanywa kwa upande wa Tanzania umeweza kubaini kuwa treni ya masafa mafupi yaani Dala Dala ifanyayo safari zake kati ya Mkamba ,Kilombero na Makambako nayo pamoja na kuendeshwa kwa mafanikio bado inakabiliwa na ongezeko kubwa la abiria kwani kwa sasa Linakokotota behewa mbili au tatu pekee badala ya behewa saba za awali na injini yake.
Hali hii imepelekea treni hiyo ya Dala Dala ya Udzungwa maarufu treni ya Mwakyembe au " Kipisi" kupakia abiria kupita uwezo wake wa kawaida kwani mizigo pamoja na abiria huchanganywa jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa abiria .
Treni hii kwa sasa uchunguzi umebaini kuwepo kwa tundu moja tu la choo kwa ajili ya huduma za Maji taka huku abiria wakitangaziwa kuwa " Abiria kabla ya kuingia ndani ya treni hakikisha unachimba dawa hapo kwenye choo cha kulipia ndani ya treni hakuna kijisaidia"
Jambo hili likiachwa liendelee kuna uwezekano mkubwa kuwaweka abiria katika Mazingira hatarishi na hivyo Serikali iangalie chanzo cha changamoto hiyo na hasa kwa kutambua treni hiyo inaendeshwa katika mfumo upi kama ni Serikali au Mtu binafsi.
Maswali ni mengi kuhusu " Kipisi " kama ni mali ya Mtu binafsi ama Serikali kwani uchunguzi wa kina uliofanywa umebaini kuwa wakati treni kubwa Wafanyakazi wanahaha na hali ngumu ya uchumi ikiwa na kuchelewa kulipwa mishahara treni ya masafa mafupi ya Udzungwa maarufu treni ya Mwakyembe au Kipisi Wafanyakazi wake wake mishahara wanalipwa na abiria wanajaa ,swali ni mali ya Umma au binafsi ?
Na kama ni mali ya Mtu binafsi iweje Wafanyakazi wa " Kipisi" tiketi na miundo mbinu pamoja na Wafanyakazi viwe chini ya Shirika ? Na kama ni mali ya Shirika kwanini wanao nufaika ni binafsi na sio wote?
Vizuri uchunguzi wa kina ukafanyika ndani ya Shirika katika treni za Kilimanjaro , Udzungwa na Ile ya Mwakanga Dar es salaam zinazo itwa Dala Dala maarufu kwa treni za Mwakyembe ili kuzibani mfumo wa uendeshaji wake nani anaziendesha Serikali au Mtu binafsi! na iweje idaiwe linajiendesha kwa hasara ili hali zinaonekana zikifanyakazi?
Nini kinasababisha TAZARA kudaiwa kuwa inajiendesha kwa hasara ? Ni Serikali kulitelekeza Shirika au ni Watu wachache kujimilikisha TAZARA bila Serikali kugundua ?
Nini kinapelekea Shirika kusua sua ? Wataalamu wetu Wasomi wanataka kutuambia kuwa wanalihujumu Shirika ? Hivi hawa abiria wanasafirishwa wakiwa wanesongamana kwenye mabehewa nao wanasafirishwa bila kulipa nauli na kusababiisha TAZARA kudaiwa kujiendesha kwa hasara au kuna mirija inayofyonza raslimali za Umma ikiamini Serikali Iko rikizo ?
Inaweza kuwa nawaza na kufikiri tofauti kuwa TAZARA inakwenda kufa kumbe ni Watu wachache ambao wanataka kuiua kwa maslahi yao binafsi , Hivyo naiomba Serikali kuinusuru TAZARA kwa kuisimamia kwa kujenga na kuboresha miundo mbinu iliyochakaa reli pamoja na mabehewa yake.
Reli ya Uhuru ya TAZARA ni tunu ilindwe na kutunzwa badala ya kuhujumiwa na kuliwa na Wajanja wachache wasio na Uzalendo wa kweli kwenye mali za Umma. " Uchunguzi unaendelea kubaini panapovuja ndani ya Shirika la TAZARA.
0 Comments