Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Wakazi wa Kata ya Hedaru, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mto Washi, mradi uliomaliza changamoto sugu ya mafuriko yaliyokuwa yakisababisha vifo vya watu, uharibifu wa mali, mazao na kukatika kwa mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Shukrani hizo zimetolewa kufuatia kukamilika kikamilifu kwa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo tarehe 28 Novemba 2025. Maagizo hayo yalihusisha uwekaji wa alama za barabarani, taa za barabarani pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji kwa lengo la kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara na kudhibiti mafuriko yaliyokuwa yakikumba eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo hayo uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Mhandisi Benitho Mnzovela, amesema kuwa maagizo yote yametekelezwa kikamilifu na mradi umekamilika kwa asilimia 100.
Baada ya ukaguzi huo, Mhe. Kasilda Mgeni ameonesha kuridhishwa na kazi iliyofanywa na TANROADS, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi kwa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu ya barabara, hususan katika eneo hilo lililokuwa likikabiliwa na changamoto na kiusalama kutokana na mafuriko.
“Mradi huu umetumia fedha nyingi za Serikali zaidi ya shilingi bilioni 1.5, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuutunza na kuilinda kwa wivu mkubwa. Daraja hili ni mkombozi mkubwa kwani limeondoa hatari ya mafuriko yaliyokuwa yakisababisha vifo, uharibifu wa mali na kukatika kwa mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Kilimanjaro na Tanga,” amesema Mhe. Kasilda.
Aidha, amewataka wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka husika endapo watabaini viashiria vya wizi au uharibifu wa alama za barabarani, taa au miundombinu ya daraja, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa wananchi na kuhujumu jitihada za Serikali katika kuwaletea maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Katibu wa Uenezi wa chama hicho, Ndg. Mohamed Ifanda, ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa daraja hilo pamoja na uongozi wa wilaya kwa usimamizi madhubuti wa mradi, akisisitiza kuwa chama kitaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Hedaru, Mhe. Herman Kajiru, amesema kukamilika kwa daraja hilo pamoja na miundombinu yake kumeongeza usalama kwa watumiaji wa barabara, kurahisisha mawasiliano na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Hedaru na maeneo ya jirani.










0 Comments