Header Ads Widget

MAENDELEO YA SAYANSI NA TECHNOLOJIA YAENDELEA KULETA MABADILIKO CHANYA



Na Hamida Ramadhan Matukio Daima app Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama


ameomba wanawake kuendelea kuliombea Taifa na kuombea kizazi kilichopo na kizazi kijacho ili kiendelee kuwa na hofu ya Mungu.

Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia Kongamano la Wanawake wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania ambalo limefanyika Sasaba Jijini Dar es salaam tarehe 31/05/2024 likiongozwa na kauli Mbiu, yake inayosema, Mwanamke ni Jeshi kubwa kwa Kanisa na Taifa.


Ameeleza kwamba mabadiliko ya Sayansi na Technolojia yanapaswa kuendelea kutusaidia kumjua Mungu kwa haraka na hayapaswi kutuingiza kwenye changamoto za kidunia. Licha ya kwamba nchi yetu haiegemei upande wowote katika masuala ya dini (Secular State) lakini sehemu kubwa ya watu wake wanaamini katika Mungu kupitia dini na madhehebu mbalimbali.


“Tukifanya kazi hii vizuri tutakuwa tumelitendea haki Taifa, na naomba niendelee kutoa wito kwa wakinamama na watoto (CPCT) muendelee kubaki imara kwenye kanisa na Taifa letu,” alihimiza Waziri Mhagama.


Waziri Mhagama amezungumzia pia uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo ametoa rai kwa wakinamama kuombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, ili chaguzi hizo zipite salama na tushawishi wanawake wenye uwezo wagombee.


“Mwanamke akipata nafasi ya kuongoza Kijiji au Mtaa na akiwa ametoka kwenye Jeshi kubwa la kuliombea Taifa atafanya kazi weledi,” alitanabaisha


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Mhashamu Askofu Dkt. Barnabas Mtokambali Amesema umoja huo uliundwa na Hayati Ali Hassani Mwinyi aliyekuwa Raisi wa awamu ya pili ambaye aliridhia kuundwa kwa Umoja wa Baraza hilo mwaka 1993 na Makao yake Makuu yalikuwa Jijini Dar es Salaam.


“Baraza hili linabaraka zote za madhebu ya kipentekoste na Baraka za Nchi na tumeunda Idara na Mabaraza kwenye ngazi za Mikoa na Wilaya ikiwemo Idara hii ya wanawake ambayo inatimiza maono, na dhima iliyokusudiwa alisema,” Mhashamu Askofu Dkt. Barnabas Mtokambali. 

Ikumbukwe Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) limetimiza miaka 31 tangu kuundwa kwake, na lina idara 9 ikiwemo Idara ya Wanawake wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania lenye maono ya kuwa na wanawake wa Kipentekoste wanaotembea katika nguvu ya Roho Mtakatifu na kuubadilisha ulimwengu kwa Injili ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, na hili ni Kongamano la kwanza la Wanawake wa CPCT Taifa kufanyika.




 MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI