Na Fadhili Abdallah,Kigoma
TUME ya Taifa ya uchaguzi imewataka viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kufuata sheria,Kanuni na taratibu za uchaguzi zilizowekwa ili kuwasilisha malalamiko yao badala ya kufanya vurugu ambazo zitasababisha kuvuruga zoezi la uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania INEC , Jaji Jacobs Mwambegele alisema hayo katika mkutano wa wadau wa Uchaguzi wa mkoa Kigoma na tume hiyo kuelekea uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura utakaofanyika mkoani Kigoma Julai Mosi mwaka huu ambapo Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa anataraia kuwa mgeni rasmi..
Jaji Mwambegele alisema kuwa tume imejipanga kuhakikisha inashughulikia malalamiko yote ambayo yatapokelewa kutoka kwa wadau wote wa uchaguzi na kwa kuanza na zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura amewataka wadau wote wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuboresha taarifa zao.
Mwenyekiti huyo wa tume ya uchaguzi alisema kuwa tofauti na mwaka 2015 na mwaka 2020 alibainisha kuwa uandikishaji wa mwaka huu umefanyiwa maboresho makubwa ikiwemo matumizi ya mfumo wa kisasa wa kidijitali na amewatoa wasiwasi wadau wote kwamba mwaka huu hawatachelewa vituoni wakati wa kuandikishaji kwani wanaweza kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao kwa kutumia simu zao za mkononi na vifaa vingine walivyo navyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa INEC,Ramadhani Kailima amesema kuwa taratibu kwa ajili ya uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura yamekamilika huku akiwataka wananchi na wadau wote kujitokeza kuboresha taarifa zao ili waweze kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi mkuu.
Sambamba na hilo Kailimi amewaonya viongozi wa vyama vya siasa, wananchi, waandishi wa Habari na wadau wengine wa uchaguzi kuacha kutoa maneno ya upotoshaji kuhusu uhalali wa wajumbe wa tume, sheria na taratibu za uchaguzi kwani kila kitu kinatekelezwa kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria za uchaguzi zilizopo.
Pamoja na hilo Mkurugenzi huyo wa Tume Huru ya uchaguzi nchini amewataka wadau wa siasa na viongozi wa dini kutumia majukwaa yao na nafasi zao kwenye jamii kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi la uboresha wa taarifa za mpiga kura.
Wakitoa maoni yao kwenye mkutano huo wadau wa uchaguzi akiwemo Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Green Shadow, Ignus Kilongola ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi kutenga bajeti kwa ajili ya asasi za kiraia kutoa elimu ya uchaguzi na ukamasishaji jamii masuala ya uchaguzi badala ya suala hilo kuachiwa asasi zitafute fedha zenyewe.
Kwa upande Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo mkoa Kigoma, Yunus Luhonvya amesema kuwa ni muhimu Tume Huru ya uchaguzi kuangalia kipengele cha kulipa mawakala wakati wa zoezi la uboreshaji wa daftari na wakati wa upigaji kura kwani vyama vingi vya siasa havina uwezo wa kugharamia mawakala kutoka kwenye vyama vyao.
Mwisho.
0 Comments