Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WATU watano watumishi wa kampuni ya Tropical State Grid Co.Ltd inayotekeleza mradi wa umeme vijijini wilayani Uvinza mkoani Kigoma wamefariki dunia na wengine wanane wamejeruhiwa baada ya gari waliyokuwa wakitumia kuacha njia na kupinduka.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari mjini Kigoma Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu alisema kuwa ajali hiyo imetokea Juni 9 mwaka huu katika Kijiji cha Rukoma wakati watumishi hao waliokuwa wakitekeleza mradi wa REA walipokuwa wakiendelea na shughuli zao.
Kamanda Makungu alisema kuwa ajali hiyo imetokea baada ya gari wanayotumikia wakandarasi hao kwenye shughuli zao aina ya Fuso lenye namba za usajili T 224 BZD kuachia njia na kupinduka likitoka Kijiji cha Lubisi kuelekea Kijiji cha Rukoma.
Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma amewataji waliofariki kwenye ajali hiyo kuwa ni Pamoja na Samwel Kashoka (30), Dismas Ntayomba (21), Enock Chimanguli (42), Benson Thomas (25) na Juma Bashiru (29) ambao ni mafundi.
Aidha aliwataja waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo kuwa ni Pamoja na Said Ramadhani (45), Venance Mabula (24) na Elizabeth Mero (30) Msimamizi wa mradi ambao walitibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kuwa nzuri.
Hadi sasa Kamanda Makungu alisema kuwa watu watano wamelazwa baada ya kuhamishiwa hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni kutoka kituo cha afya Rukoma wilaya ya Uvinza kutokana na hali zao kuhitaji matibabu Zaidi.
Kamanda huyo wa polisi aliwataja majeruhi ambao bado wamelazwa wakiendelea na matibabu hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni kuwa ni Pamoja na Hussein Fadhili (24), Yasini Athumani (19), Mtala Joseph (24) victor Joseph (31), Claudiao Mwalima (31)
Mwisho
0 Comments