.TAZAMA TUKIO ZIMA KUPITIA VIDEO HI BOFYA LINK
NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Dkt.Tulia Ackson amekabidhi matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita elfu tano kila tenki ili kusaidia kuboresha huduma katika kituo cha afya Itagano jijini Mbeya.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi matenki hayo, mganga mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Dr. Yesaya Mwasubila kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji hilo John Nchimbi, amesema baadhi ya vifaa tiba vilikuwa bado havijapatikana lakini tayari vimeshaletwa ikiwemo jenereta kwa ajili ya nishati ya umeme.
"Kwakweli tumshukuru sana Dkt.Tulia kwani pia hatukua na tenki la maji ambayo aliahidi Mhe. Mbunge (Dkt. Tulia Ackson) ambayo ameyatoa lakini pia fedha zaidi ya Million ishirini zimetolewa ili kulipa madeni yaliyokuwa yamesalia na kumalizia baadhi ya kazi ambazo zilikuwa zimesalia hapa kituoni ili huduma za upasuaji zianze kutolewa hapa na niwaombe tu wananchi wa Itagano tuvute subira kidogo tu", amesema Dr. Mwasubila.
Aidha amesema Serikali kupitia Wizara ya afya inajipanga kuongeza watumishi kituoni hapo hivyo kuwaomba wananchi kuvuta subira ndani ya muda mfupi usiozidi miezi miwili kuhakikisha wanakamilisha miundombinu ya kituo hicho cha afya.
John Mboya ni Afisa tarafa ya Sisimba jijini Mbeya, akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Benno Malisa, amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kwenye afya kwa maslahi ya jamii hivyo kumpongeza Mbunge Tulia Ackson kwa kuwa na moyo wa kuwapenda wananchi wake hususani katika miradi ya Elimu, afya na Maji.
Ofisa kutoka idara ya habari na mawasiliano ya taasisi ya Tulia Trust Addy Kalinjila, ndiye amekabidhi matenki hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tulia Trust ambapo amesema pia pamoja na hayo wamepanda miti kumi ya matunda kwenye eneo hilo la kituo cha afya Itagano ili kuhifadhi mazingira na kuwaomba viongozi na wananchi wa eneo hilo kutumia vizuri uboreshaji miundombinu hiyo.
Naye Diwani wa Kata ya Itagano Mhe. Yuda Aron Sikawenga, amemshukuru Mbunge wake Mhe. Dkt. Tulia Ackson kwa kutekeleza ahadi ya matenki kwenye kituo cha afya Itagano.
Pia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya idara ya afya kwenye kituo hicho ambacho kinatoa dira ya kuanza kutumika kwa huduma za upasuaji kwenye kituo hicho kipya ambacho kiko pembezoni mwa jiji la Mbeya na Jimbo la Mbeya vijijini.
Kituo cha afya Itagano jijini Mbeya kilijengwa na Serikali kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2022 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Million miatano ikiwemo kwa fedha za tozo ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kituo cha afya Ruanda Mwanjelwa ambapo huduma ambazo bado zinasubiriwa na wananchi ni pamoja na huduma za upasuaji na huduma za afya ya uzazi (huduma ya baba, mama na mtoto).
0 Comments