Na Moses Ng'wat, Mbozi.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe, kukutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ardhini (Latra) ili kutengeneza mpangilio wa shughuli za usafirishaji kati ya Miji ya Vwawa na Mlowo, Wilayani humo.
Ametoa maagizo hayo leo Juni 6, 2024 mara baada ya kutembelea na kufanya kukagua wa ukamilishaji wa stendi ya magari ya abiria ya Mlowo na kupokea malalamiko kutoka kwa madereva wa daladala.
Mmoja wa madereva hao wa daladala, Daniel Mbusa, alilalamikia bajaji kufanya shughuli zao bila mpangilio, hali ambayo imesababisha utendaji kazi wa Daladala kuwa mgumu kati ya miji ya Vwawa na Mlowo.
Kufuatia malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa Chongolo alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, kukutana haraka na Mamlaka ya Udhibiti wa Ardhini (Latra) ili kuweka mpangilio mzuri wa shughuli hizo za usafirishaji wa abiria katika miji hiyo.
"Mkuu wa Wilaya naomba mkutane na Mamlaka ya Udhibiti wa Ardhini (Latra) kwa ajili ya kutengeneza utaratibu na uratibu mzuri wa shughuli za usafirishaji aburia ili kila mtu aweze kufanya kazi na kupata ridhiki" aliagiza Chongolo.
Aidha, Chongolo ameuagiza uongozi wa Halmashari ya Mbozi kuendelea kufanya maboresha ya miundombinu ndani ya stendi hiyo, ikiwemo kuwekwa kokoto ili kuzuia vumbi, vihifadhia taka, taa, pamoja na mlinzi.
Vilevile, Chongolo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga, kuhakikisha anasimamia magari yote ya abiria kufanya shughuli zake kwa kufuata taratibu kwa mujibu wa leseni zao, ikiwemo kuingia ndani ya stendi hiyo kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria na si vinginevyo.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mahawe alisema kuwa zoezi la uratibu wa wafanyabiashara kumalizia ujenzi wa vibanda hivyo unaendelea vizuri ambapo wamiliki wa vibanda 226 wamekubaliana kufikia maridhiano ya kuunganisha vibanda kutokana na udogo wa vyumba hivyo ambapo vyumba viwili vitatoa chumba kimoja ili kufanya mazingira ya ufanyaji biashara kuwa bora ndani ya stendi hiyo.
"Mkuu wa Mkoa sisi tunaendelea na utekelezaji wa maagizo yako na tayari wamiliki 226 wa vyumba wamekubaliakuachiana vyumba kama ulivyoshauri na wameahidi kuwa kuanzia kesho wanaanza kazi ya kumalizia ujenzi ili waanze kufanyabiashara, ingawa bado kuna wengine 30 tunaendelea nao, lakini kwa asilimia kubwa maagizo yako yametekelezwa". alieleza Mahawe.
Mei 14,2024 mkuu wa mchongolo alitembelea stendi hiyo, na kukutana na wamiliki wa vyumba vya biashara na kushauri wamiliki hao kukaa pamoja na kukubaliana kuunganisha vibanda kutoka vibanda viwili kuwa kimoja baada ya vile vya awali kuonekana kuwa ni vidogo hali iliyolalamikiwa na wafanyabiashara hao.
Mwisho.
0 Comments