Header Ads Widget

CCM SINGIDA YAKIPONGEZA KIWANDA CHA BIOSUSTAIN KUJENGWA MABWENI IRAMBA

 






Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimekipongeza Kiwanda cha Pamba cha Biosustain kilichopo Manispaa ya Singida kwa kufanikisha ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari ya Mtekente iliyopo wilayani Iramba ambalo limegharima zaidi ya Sh.milioni 180.


Kiwanda hicho kimejenga bweni lenye uwezo wa kupokea wanafunzi 80,jiko na kisima kwa fedha zake.


Katibu wa Siasa na Uenezi CCM Mkoa wa Singida, Elphas Lwanji,ametoa pongezi hizo jana (Juni 29, 2024) baada ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Mipango na Uwekezaji,Prof.Kitila Mkumbo alipotembelea kiwanda hicho kinachomilikiwa na wazawa kuangalia shughuli za uzalishaji zinavyofanywa.


Pongezi hizo za CCM zimekuja ikiwa ni takribani wiki tatu baada Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego, alipotembelea Juni 11, 2024  bweni hilo lililojengwa katika Shule ya Sekondari Mtekente na kukataa kulizindua kwa kile alichoeleza kuwa umaliziaji (finishing) haikuwa nzuri.


"CCM inawapongeza kampuni ya Biosustain hapa Singida tumeona mnavyofanya kazi,mnatoa ajira kwa wananchi huko vijijini mnawapa fedha za pamba kwa wakati wakulima na juzi juzi wamejenga mradi mkubwa wa bweni kwa ajili ya watoto wetu huko Iramba ambalo litasaidia watoto wa wafugaji na wakulima waweze kufikia malengo yao ya elimu," alisema.


Lwanji alisema CCM imeridhika na namna kiwanda hicho cha pamba kinavyofanya kazi katika sekta ya viwanda na ndio maana kiwanda kimendeelea kuwepo na kuendelea na uzalishaji hadi sasa na kutoa ajira kwa wananchi wengi.


"Sisi kama CCM kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,Martha Mlata,tunakupongeza Mkurugenzi kwa ushirikiano mkubwa unaotoa kwa chama, na mheshimiwa Waziri hawa (Biosustain) ni wadau wetu muhimu wakubwa sana kwenye chama chetu tunapokuwa na mambo mbalimbali ya kufanya wanatusaidia," alisema Lwanji.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho, Sajjad Haider, alisema mwaka huu kiwanda kimechukua mkopo wa takribani Dola za Kimarekani milioni 14 kwa ajili ya kuendelea na uzalishaji katika kiwanda hicho.


Naye Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Mipango na Uwekezaji, Prof.Kitila Mkumbo, alisema serikali inafurahishwa na uwekezani unaofanyika katika kiwanda hicho kwasababu fedha zinazokopwa zinaingia kwenye mzunguko wa uchumi wa Mkoa wa Singida.


"Umuhimu wa viwanda ni kusaidia kunyenyua pato la Mkoa wa Singida sasa nyie mnapokopa fedha sisi hilo ndio muhimu maana tunahesabu 'value' ya kuingia kwenye uchumi wa mkoa wetu wa Singida," alisema Prof.Mkumbo.


Prof.Mkumbo alisema serikali inahamasisha uchakataji wa mazao ya wakulima ya nafaka na chakula hususani katika zao la Pamba ambalo linalimwa katika mikoa 17.


"Karibu nusu ya idadi ya wakulima wanategemea zao la pamba lakini changamoto iliyopo ni kwamba asilimia 80 ya pamba inayozalishwa Tanzania inauzwa kama malighafi kabla haijachakatwa," alisema Prof.Mkumbo.


Alisema nia ya rais na serikali kwa ujumla ni kuona angalau kiwango cha kuchakata pamba kinafikia kati na kiwanda cha Biosustain kiwe ndio mfano ili pamba isiwe inauzwa kama malighafi hali ambayo inasababisha watu kukosa ajira.


"Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano ili kupunguza usafirishaji wa pamba nje ya nchi ikiwa katika hali ya ambayo ni ghafi,kuchakata pamba nchini kuna uwezekano mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi," alisema Prof.Mkumbo.


Aidha,Prof.Mkumbo alisema serikali ipo katika hatua za kushughulikia changamoto za EFD ambapo inapitia upya mfumo wa kodi nchini na eneo linaloangaliwa ni la EFD.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI