Kijana Innocent Chengula aliyemtapeli Ridhiwani Kikwete akipelekwa jela
Mhe Ridhiwan Kikwete
Na Matukio Maima App
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imemhukumu Innocent Chengula (23),kwenda jela miaka saba na kumlipa fidia ya Sh. milioni nne Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete baada ya kukutwa na hatia ya kujipatia kwa njia ya udanganyifu fedha hizo.
Kadhalika mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga imetaifisha simu moja ya mkononi na laini tatu za mitandao ya simu baada ya kuzitumia kujitambulisha kwa Kikwete kuwa ni Dk. Hassan Abbas ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hakimu alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri bila kuacha shaka imethibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
“Mshtakiwa utakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka saba, kumlipa fidia ya Sh. milioni nne Naibu Waziri Kikwete, simu moja na laini tatu za simu ya mkononi zinataifishwa kuwa mali ya serikali ili iwe fundisho kwa wenye tabia kama ya mshtakiwa” alisema Hakimu Ruboroga wakati akisoma hukumu hiyo.
Hukumu hiyo imesomwa leo Juni 5, 2024 baada ya kesi hiyo kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa dhidi ya mashtaka sita yaliyokuwa yanamkabili Chengula ambaye pia ni mkazi wa Kigogo Luhanga jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka sita ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kupitia ujumbe wa maandishi kwenda katika mtandao wa Whatsapp akijitambulisha kuwa ni Dk. Abbas wakati akijua ni kosa kisheria.
Mwisho
0 Comments