Na Matukio Maima App
WAKAZI 12 wa Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 50 ikiwamo kutuma ujumbe mfupi kwenye simu za watu tofauti, kuwashawaishi wajiunge na chama cha Freemason Tanzania na kujitambulisha kuwa ni waganga wa kienyeji wanasafisha nyota.
Washtakiwa hao ni, Pius Mahali (29) dereva, Best Shinyangwe (24) dereva bodaboda, Andrea Kipeta (31) mkulima, Lusekelo Jimmy (32), Michael Donati (28), Lucas Mpanduzi (19), Steven Seleman (18), Emmanuel Kawimbe (30), Alvin Mbingi (30), Charles Selaman (20), Fabian Dismas (18) na Alex Tungombe (27)(wote waliyobaki ni wakulima).
Upande wa Jamhuti uliongozwa na Wakili wa Serikali, Eric Kamala akisadiana na Aaron Titus ulidai leo Juni 5, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kwa mashtaka 50, moja la kuongoza genge la uhalifu, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu 19, kutuma sms za ushawishi 12, kutumia laini zilizosajiliwa kwa majina mengine 17 na utakatishaji fedha moja.
Kamala alidai kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo mwaka 2023 na mwaka 2024 katika maeneo yasiyofahamika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakituma ujumbe ufupi kwenye simu za watu na kisha kujipatia fedha Sh milioni 9.2 kutoka kwa watu mbalimbali na mawakala wakijifanya wao ni waganga wa kienyeji.
Alidai kuwa Mahali anatuhumiwa Desemba 19,2023 alimtumia mtu ujumbe kuwa, "Mjukuu wangu nimekusaidia sana mpaka sasa una majumba magari ya kifa Alidai kuwa Mahali anatuhumiwa Desemba 19,2023 alimtumia mtu ujumbe kuwa, "Mjukuu wangu nimekusaidia sana mpaka sasa una majumba magari ya kifahari lakini hatakuja kunishukuru hujawahi, nizirudishe mali kwenye mizimu? Basi nakutakia utajiri mwema"
Ujumbe mwingine, mshtakiwa Shinyangwe aliutuma kwenda kwa Samwel Kiwembe Mei 6, 2024 kwamba, "Leo una kufa majini yamekasirika sana".
Pia, Mshtakiwa huyo siku hiyo alituma ujumbe mwingine kwenye namba ya simu 0697 590144 kwamba, " Binti kuna shida inaenda kukutokea leo muda wa jioni,"
Naye mshtakiwa watano, Kipeta alituma ujumbe kwenye namba mbili tofauti akieleza kwamba, "(666) Jiunge na chma huru cha Freemason Tanzania umiliki mali pesa majumba mvuto vipaji pete bila kafala kwa kujiunga PG 0772 981316,".
Kamala aliendelea kusoma jumbe hizo kuwa, mshtakiwa wanane Mpanduzi anatuhumiwa Machi 10,2024 kutuma ujumbe unaoeleza kuwa, "Mjukuu wa Kisile naona biashara ya mabasi sasa inatosha umeshanunua mabasi mengi, sasa uje tena Sumbawanga nikupe dawa ya kusafisha nyota na ya ndagu mimi ni babu yako wa Sumbawanga mzee Ramadhani,".
Alidai kuwa mshtakiwa Kawimbei anatuhumiwa Januari Mosi, 2024 akiwa eneo na mkoa usiohafamika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alituma ujumbe mfupi kuwa, " Kaka nashukuru sana kwa mtaalamu aliyeniletea kwani kwasasa. Na ajabu leo asubuhi tumewakuta wale wezi walioiba vile vitu getini wakiwa wamevibeba vyote sasa nakuomba sana tena kwa ustazi kamwambie kuwa nimpe nini kama zawadi? Pls jib".
Pia, wakili huyo alidai kuwa Mahali na Shinyangwe wanatuhumiwa Mei 7,2024 wakiwa eneo la Edeni A ndani ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa walitumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine Sarafina Haonga, Noelia Nachipeta, Asma Nguche, Lameck Kiliwa, Manza Sandala, Andrew Leo na Katalina Nampamba.
Washtakiwa wengine wanaoshtakiwa na shtaka hilo ni Jimmy, Donati, Mpanduzi, Seleman, Tung'ombe, Mbingi na Kawimbe ambao walitenda kosa hilo Mei 7, 2024 maeneo ya Kashai na Edeni A, Sumbawanga.
Pia, katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu yanamkabili Mahali, Kipeta, Seleman, Mbingi ambao wanatuhumiwa kujipatia fedha kutoka kwa watu mbalimbali na mawakala wakijitambulisha kuwa wao ni waganga wa kienyeji wakati si kweli.
Kamala alidai kuwa makosa hayo waliyatenda mwaka jana Septemba na Desemba na kwa mwaka huu waliyatenda mwezi Januari, Februari na Aprili, ambapo walijipatia Sh milioni 9.2.
Katika shtaka la 49, Aaron alidai kuwa washtakiwa wote wanatuhumiwa kati ya Septemba Mosi, 2023 na Mei 5,2024 walijipatia Sh milioni 9.2 kutoka kwa watu mbalimbali kwa madai kuwa wao ni waganga wa kienyeji huku wakijua si kweli.
Shtaka la 50, linawakabili washtakiwa wote ambapo wanatuhumiwa kati ya Septemba Mosi, 2023 na Mei 5, 2024 walijipatia fedha hizo huku wakijua ni mazalia ya uhalifu ambalo ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu kesi wanayotuhumiwa nayo ni ya uhujumu uchumi na pia shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana kisheria, kwa hiyo Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Kesi imeahirishwa hadi Julai 27, 2024 washtakiwa wamerudishwa mahabusu.
Mwisho
0 Comments