Header Ads Widget

MBARONI KWA MAKOSA YA UTAPELI, UNYANYASAJI, UNAJISI WA MTOTO (02) SONGWE.

 


Na Matukio Maima App 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kipindi cha mwezi Mei, 2024 limewatia nguvuni watuhumiwa 680 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya ukatili wa kijinsia, uvunjaji, wizi, mauaji, utapeli kwa njia ya mtandao, dawa za kulevya, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali za vifo.


Pia jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia wanaume wawili (02) ambao ni wakazi wa Kaloleni Wilaya ya Songwe wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini kwa tuhuma za kumnajisi na kumuua mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili na nusu mkazi wa kaloleni Wilayani humo.


Watuhumiwa hao walifanya tukio hilo kwa kumchukua mtoto huyo na kwenda kumbaka kwenye shamba la mahindi umbali wa mita 130 mnamo Mei 09, 2024 kutoka nyumbani kwao baada ya kuachwa na mama yake mzazi akiwa amelala huku mama yake akienda kuchota maji kisimani.



Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe kamishna msaidizi SACP Augustino Senga, uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mauaji hayo yametokana na imani za kishirikina kutokana na shughuli za watuhumiwa za uchimbaji wa madini.


Kamanda Senga anasema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo ziliripotiwa katika kituo cha Polisi tarehe 09 Mei, 2024 na tarehe 10 Mei, 2024 kubainika akiwa ameuawa.


Kamanda anasema upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea na pindi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.


Vilevile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia mke na hawara yake kwa tuhuma za mauaji ya mumewe kutokana na wivu wa kimapenzi.


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe Augustino Senga amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua Victor Mwakapenda (41) mkazi wa Mtaa wa llembo Wilaya ya Mbozi ambapo marehemu alitoweka nyumbani tangu Aprili 30, 2024 akiwa na mke wake wanaelekea kwa mganga wa kienyeji  eneo la Senjele Majimoto Wilayani Mbozi na mwili wake ulipatikana Mei 9, 2024 katika msitu wa Mpoloto uliopo Kijiji cha Igale Wilayani Mbeya. 


Aidha mwili huo ulitelekezwa katika msitu huo na kuonekana na wananchi waishio maeneo hayo na kisha taarifa zilitolewa na JeshI la Polisi kuuchukua na kuupeleka hospitali ya Ifisi jijini Mbeya na kuhifadhiwa mpaka ndugu zake walipoutambua Mei 29, 2024 na kukabidhiwa kwa ajili ya mazishi.


Upelelezi wa shauri hilo pia bado unaendelea na pindi utakapokamilika Polisi Mkoa wa Songwe inasema watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.


Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe katika kipindi cha mwezi Mei, 2024 limeendelea kupata mafanikio mahakamani kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali kuhukumiwa ambapo jumla ya watuhumiwa 12 wamepatikana na hatia na kufungwa gerezani wakiwemo watuhuniwa watatu waliofikishwa mahakamani kwa makosa tofauti ambapo Osea David Clement Simwanza (32) kosa la kuzini na ndugu yake wa damu (kuzini na maharimu) kesi namba 202/2023 na Ngasa Shija Maige (25) pamoja na Simon Salati Mwakasula (30) walifikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka kesi namba 70/2023 na 3985/2024 na kuhukumiwa miaka 30 jela katika mahakama ya Wilaya ya Momba na Songwe kila mmoja.


Mtuhumiwa Yohana Loti Mwashala (36) alifikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi kesi namba 04627/2024 na kuhukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kubaka na miaka 20 jela kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi.


Mtuhumiwa Baraka Watson Kameme (28) alifikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi kwa kesi namba 61/2023 na kuhukumiwa miaka 30 jela kwa kesi ya kubaka na miaka 03 jela kwa kesi ya kumpa mimba mwanafunzi katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi.


Mtuhumiwa Sikujua George Mwilenga (32) alifikishwa mahakamani kwa kosa la wizi kesi namba 9694/2024 na kuhukumiwa miaka 07 jela katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi.


Mtuhumiwa Yusuph Laiton Simbeye (28) alifikishwa mahakamani kwa kosa la kufanya mapenzi na mtu asiye na akili timamu kesi namba 11722/2024 na kuhukumiwa miaka 10 jela katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi.


Mtuhumiwa Nione Litson Kapesa (35) na wenzake wawili walifikishwa mahakamani kwa kosa la wizi kesi namba 06/2023 na wamehukumiwa miaka 05 jela katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi kila mmoja.


Mtuhumiwa Timoth Michael Kamendu (29) alifikishwa mahakamani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kesi namba 38954/2023 na kuhukumiwa miaka 08 jela katika mahakama ya Wilaya ya Momba kila mmoja.


Mtuhumiwa Ibrahim Reginald Kisamo (34) alifikishwa mahakamani kwa kosa la kughushi kesi namba 06/2023 na kuhukumiwa miaka 03 jela katika mahakama ya Wilaya ya Songwe.


Katika muendelezo wa misako dhidi ya dawa za kulevya jumla ya watuhumiwa 08 walikamatwa na dawa za kulevya aina ya bhangi gramu 8.5 na bidhaa za magendo zenye thamani ya zaidi ya Tshs.3,870,000/= ikiwemo sukari aina ya whitespoon za Zambia, Pia katika msako huo walikamatwa watuhumiwa 04 wanawake wakiwa na lita 32 za Pombe ya Moshi (gongo) watuhumiwa watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapo kamilika.


Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia watuhumiwa 8 kwa makosa ya wizi wa pikipiki 32 za kampuni aina mbalimbali zilizokamatwa Wilayani Mbozi 07, Momba 11 na Songwe 14  katika operesheni na misako na kukutwa hazina plate namba pia watuhumiwa 25 wamekamatwa kwa makosa ya uvunjaji na upelelezi wa baadhi ya kesi hizi umekamilika na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.


Sambamba na hayo, kwa kipindi cha mwezi Mei, 2024 jumla ya makosa mbalimbali ya usalama barabarani 4,716 yalibainika na baadhi ya watuhumiwa walifikishwa mahakamani, wengine kulipa faini na dereva 01 aitwaye Daniel Michael Ki mkazi wa Mbeya nwenye umri wa miaka 41 amefungiwa leseni kwa makosa ya mwendokasi.


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani humo linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe ambao wanajihusisha na uhalifu na vitendo vya ukatili wa kijinsia kuacha mara moja kwani hawatoweza kukwepa mkono wa sheria.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI