Header Ads Widget

WAZAZI, WALEZI WAASWA KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO



Wananchi Wilayani Mbozi Mkoani Songwe wametakiwa kusimamia maadili ya watoto wao ili kujenga kizazi chenye maadili mema kwa manufaa ya taifa la sasa na baadaye.


Kauli hiyo imetolewa Mei 30, 2024 na Polisi Kata wa kata ya Mlangali Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Robert Kasunga, wakati akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa kijiji cha Lukululu Kata ya Mlangali kwa lengo la kutoa elimu ya Polisi Jamii na umuhimu malezi bora kwa watoto.


Kasunga amesema “Ni lazima kuwajenga watoto kiimani kwa kuwataka waende kwenye nyumba za ibada ili wamjue Mungu na kuwa na hofu ya Mungu ikiwemo kuwapeleka kwa bibi na babu zao ili waweze kufundishwa yale yote yaliyo mema katika mila na desturi zetu za kitanzania kwa lengo la kuondokana na tamaduni za nje ambazo kwa sasa zina waathiri sana watoto wetu”, amesema Mkaguzi Kasunga.


Sambamba na hilo, pia wananchi hao wamesisitizwa kuzingatia suala la utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia matukio ya kihalifu kupitia dhana ya ulinzi shirikishi na ulinzi jirani.


Kwa sasa Jeshi la Polisi linafanya kazi kisasa kwa kushirikiana na wananchi na kujenga urafiki ili kuhakikisha kwa pamoja vitendo vya uhalifu na wahalifu na matukio ya ukatili na unyanyasaji vinakomeshwa kwa mstakabali bora wa kizazi cha leo na kesho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI