Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye akizungumza kwenye mkutano na walengwa wa mpango wa kusaidia kaya masikini katika kijiji cha Chakuru wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amewataka walengwa wa mpango wa kuinua kaya masikini (TASAF) kutumia fedha zinazotolewa kwao kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwenye maisha yao ni kuunga mkono maono ya Raisi Samia Suluhu Hassan katika kupunguza umasikini kwa Watanzania.
Andengenye alisema hayo akizungumza na walengwa wa mpango huo katika Kijiji cha Chakuru wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma akiwa kwenye ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya wananchi mkoani humo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa mpango wa TASAF unayo maono na malengo makubwa katika kuinua kipato cha Mtanzania na kuwaondoa katika hali ya umasikini na kwamba fedha zinazotolewa kwa walengwa lazima zizingatie miongozo hiyo sambamba na walengwa kutumia sehemu ya fedha hizo kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi
Awali Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Chakuru, Mathias Ndimkanwa akitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa Kigoma alisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 28.3 kimetumika kwa walengwa wa TASAF kwenye Kijiji hicho tangu mwaka 2021 ambapo kwa sasa Kijiji kina walengwa 40.
Mtendaji huyo wa Kijiji cha Chakuru alisema kuwa katika muda huo na fedha hizo zilizotolewa kwa walengwa wengi wao wameweza kuzitumia na kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwenye Maisha yao ikiwemo kujenga nyumba bora na kati yao 12 wameweza kuanzisha miradi ya ufugaji kuku ambapo kuku Zaidi ya 100 wameweza kutotolewa.
Mmoja wa walengwa wa mpango huo, Maira Mabuga alisema kuwa fedha hizo zimewezesha wangi wao kuanzisha miradi ya kiuchumi ambayo imewezesha kuongeza kipato cha familia ambapo Pamoja na hilo ameiomba serikali kuwaongeza kiwango cha pesa kinachotolewa hasa kwenye kazi za ajira za muda.
0 Comments