Header Ads Widget

WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU, TAS NA THRDC WALAANI TUKIO LA KUSHAMBULIWA KWA MTOTO MWENYE UALIBINO GEITA

Chama cha Watu wenye Ualibino Tanzania (TAS) pamoja na Mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu (THRDC) wameelaani vikali tukio kudaiwa kuvamiwa na kushambuliwa kwa mtoto mwenye ualibino mkoani Geita, ambapo wametoa wito kuwachukulia hatua za kisheria haraka kwa watakaobainika kuhusika.

Tukio hilo linalodaiwa kutokea Mei, 2024 ambapo inadaiwa kazungu alivamiwa na kukatwa mapanga kwenye uso akiwa anachota maji karibu na nyumbani kwao.

Tamko hilo limesomwa na Mwenyekiti TAS, Abdillah Omary ambaye amesema kuwa tukio hilo limemsababishia majeraha mabaya hasa kwenye mkono wa kulia na sehemu ya kichwa.

"Kitendo hiki cha kikatili dhidi ya mtoto asiye hatia sio tu cha kuchukiza bali pia kinaonyesha tamaa na ushirikina uliokithiri unaoendelea kuikumba jamii yetu na Taifa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuichafua nchi yetu" amesema Mwenyekiti TAS, Abdillah Omary

Pia katika tamko hilo wameeleza, kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Baba mzazi wa Kazungu Julius Malecha, ni kwamba wanaodaiwa kumshambulia ambao bado hawajulikani walivamia nyumba ya familia hiyo gizani na kufanya tukio hilo.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa watu hao walishindwa kutimiza azma yao baada ya Kazungu na familia yake kufanikiwa kupiga kelele na kufanya majirani kufika kuwasaidia na kuzima nia ya watuhumiwa hao, ambapo kwa taarifa hiyo inaelezwa kuwa watuhumiwa hao waliacha ndala, panga pamoja na kofia eneo la tukio.

Aidha tamko hilo limeeza "Sisi Chama cha Watu wenye Ualibino pamoja na Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu tunasimama na Kazungu Julius katika kipindi hiki kigumu. Hakuna mtoto anayestahili kufanyiwa vitendo hivi vya kikatili na kinyama kwa sababu tu ya hali au muonekano wake." 

Pamoja na wadau hao kutoa wito kwa mamlaka husika kuharakisha uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya Sheria, wadau hao wameonesha mashaka yao kufuatia kauli Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo  kuhusu uchunguzi wa awali.

Ambapo Kamanda huyo alidai kuwa "uchunguzi wa awali unaonesha kwamba tukio hili ni la kupangwa na aliyepanga hasa nia haikuwa ni kuondoka na kiungo nia ilikuwa ni kumjeruhi kwa sababu umri wa Mtoto na aina ya panga ambalo limekuwa eneo la tukio kama alikuwa na nia ya kuondoka na kiungo basi angeweza kumkamata"

Wadau hao kupitia Afsa kutoka Dawati la Watu wenye Ulemavu THRDC, Perpetua Senkoro wanadai kuwa kauli hiyo inaibua maswali yanayoleta wasiwasi kutolewa mapema hali ambayo inaongeza wasiwasi katika hatua zaidi za uchunguzi ikizingatiwa mpaka sasa bado watuhumiwa hawajatiwa mbaloni.

"Kwetu sisi tukifikiria upelelezi kwanza ndio unaanza, haujakamilika hao watu waliohusika mpaka sasahivi bado hawajakamatwa inamaana hata kuhojiwa awajahojiwa kama mtazamo wa Jeshi la Polisi katika hizi nyakati za mwanzo kabisa umeshaweka kwamba nia ya wale watu haikuwa kukata huu mkono je, huu mchakato mzima wa ukusanyaji ushahidi ambao ndio utaenda kutumika katika kutekeleza haki mahakamani je, utafanyika kwa ubora ambao unaotakiwa" amesema Perpetua Senkoro

Ameongeza kuwa historia inaonesha kwamba zipo kesi za matukio ya aina hiyo ambazo zimetupiliwa mbali kutokana na ushahidi uliojitosheleza dhidi ya watuhumiwa.

Hata hivyo wadau hao wametoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira, na Watu wenye Ulemavu, kumalizia haraka mchakato wa upitishwaji rasimu ya mpango kazi wa Taifa kwa Watu wenye Ualibino 2023/2024 - 2027/2028 ili hatua za utekelezwaji zifuate.

Sanjari na hilo wametoa rai kwa mamlaka za kisheria kuwajibisha myororo mzima wa wahusika wanaobainika hususani tukio endapo linahusishwa na ushirikina, ambapo wamesema kuwa kuwajibishwa kwa wanaoenda kwa wapiga ramli kupewa amri zisizo rafiki, wapiga ramli pamoja na watekelezaji wa matukio, wakidai kuwa kwa kufanya hivyo kutaongeza usalama kwa Watu wenye Ualibino katika jamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS