NA MATUKIO DAIMA APP ZANZIBAR
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud ameagiza viongozi wa Wilaya, Halmashauri na Mabaraza ya Miji na Manispaa kuhakikisha wanawachukulia hatua stahiki Watumishi wa Umma Wazembe, Wavivu na wale wote wanaokwenda kinyume na Sheria, Kanuni na utaratibu wa Kazi.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo hilo kufuatia kutoridhishwa na tathmini ya utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumza na Watumishi wa Umma katika uzinduzi wa Program ya Amsha Amsha timiza wajibu, amesema kuwa, ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Serikali ya awamu ya nane ni vyema kwa viongozi ndani ya mkoa huo kusimamia na kuwachukulia hatua watumishi wote wavivu, wazembe na watoro kazini.
"Kusini Unguja sasa hatutaki, Wazembe,Wavivu, Watoro na wale wote wanaotoa maneno maneno katika maeneo yao ya kazi, sasa naahidi kula nao sahani moja kwa kuwachukulia hatua zinazostahiki," amesema.
"Viongozi wote ndani ya mkoa wa kusini bila ya kumuonea mtu huruma niwaagize kuanza mara moja kuwasimamia ipasavyo Watumishi hawa wauma ili tutoe huduma bora kwa wananchi," ameongeza.
Aidha amewataka Watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
"Tunahitaji mabadiliko ndani ya mkoa wetu tufanyeni kazi kwa msingi iliyowekwa na tuendane na wakati ili kupiga hatua zaidi," ameeleza.
"Kwa wale wote watakwenda kinyume na haya maagizo tusije kulaumiana nina ahidi kusimamia yale yote niliyaagiza leo," amefafanua.
Program hiyo ya Amsha amsha timiza wajibu imezinduliwa na Katibu Mkuu Kiongozi na katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmed Saidi.
0 Comments