Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Bi. Happiness Seneda, ameongoza kilele cha maadhimisho ya siku ya Wauguzi Mkoani Songwe.
Maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika Ijumaa hii (Mei 31, 2024) katika viwanja vya CCM Vwawa Wilayani Mbozi.
Katika maadhimisho hayo, Seneda ametoa vyeti kwa wauguzi bora katika kila halmashauri za mkoa huo huku akishiriki kuchangia Damu ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizofanyika katika maadhimisho hayo.
Akizungumzia siku ya Wauguzi duniani, kiongozi huyo amesema siku hiyo huadhimishwa kwa heshima ya Wauguzi na wafanyakazi wa idara ya afya kote ulimwenguni.
Siku hii ilitengenezwa kwa heshima ya Florence Nightingale ambaye alikuwa muuguzi maarufu huko nchini uingereza na mwanzilishi wa taaluma ya uuguzi wa kisasa.
Pia, Katibu tawala huyo wa mkoa amewaagiza Wakurugenzi na Waganga wakuu Wa Halmashauri za mkoa wa Songwe kuhakikisha wanatenga fedha kuwezesha maadhimidho hayo ngazi za halmashauri na kutatua changamoto ya wauguzi kutopata posho ya sare ya kazi akisema ni takwa la kimuundo hivyo ni wajibu wa waajiri wote kuhakikisha wauguzi wao wanapatiwa posho ya sare za kazi.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Songwe Dr. Boniface Kasululu ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya idara ya afya na kuahidi kuendelea kusimamia uadilifu na nidhamu kwa wauguzi kwa matokeo bora zaidi kwa wananchi ndani na nje ya mkoa wa Songwe.
0 Comments