Header Ads Widget

MBUNGE PROF. PATRICK NDAKIDEMI AWAFARIJI WAHANGA WA MAFURIKO MABOGINI NA ARUSHA CHINI..



NA WILLIUM PAUL, MOSHI. 



MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, Prof. Patrick Ndakidemi amewatembelea wahanga wa Mafuriko katika kata za Mabogini na Arusha chini na kutoa msaada wa tani mbili za mahindi. 



Katika kata ya Mabogini jumla ya kaya 372 na kata ya Arusha chini kaya 93 zimeathirika na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha. 



Akizungumza Mbunge Ndakidemi alisema kuwa, janga hilo ni kubwa kwani limewaacha wananchi bila makazi pamoja na chakula na kudai kuwa Serikali kupitia kitengo cha maafa inaendelea kuweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia wahanga wote. 



Alisema kuwa, mafuriko hayo yamesababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwaomba wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuhama kipindi hiki ili kuepuka madhara makubwa zaidi yanayoweza kutokea kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. 



Mbunge huyo alisema kuwa, kutokana na mvua zilizonyesha barabara nyingi zimeathirika na kuwaomba wananchi kuwa na uvumilivu kipindi hiki ambacho Serikali inaweka utaratibu wa kuhakikisha inarejesha mawasiliano. 



Wakitoa taarifa fupi kwa nyakati tofauti, Diwani wa Kata ya Mabogini Dkt. Bibiana Massawe na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mikocheni Salehe Kulakwa walimthibitishia Mbunge kwamba kwenye maeneo yao hakuna vifo vilivyotokana na mafuriko hayo, bali wananchi wengi wamepoteza makazi yao, na mazao mashambani kusombwa na maji.



Wananchi walimwomba Mbunge awasaidie ili wapate maeneo ya kujenga makazi ambayo hayataathiriwa na Mafuriko. Mbunge alisema atafikisha ombi hilo kwa  viongozi wa Serikali.


Mwisho.. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI