NA WILLIUM PAUL.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Prof. Patrick Ndakidemi amesema kuwa bila maji hakuna maisha na kuitaka Wizara ya Maji kuja na mpango kazi wa maji ili kupambana na upungufu wa maji unaotarajiwa kuja miaka kumi ijayo.
Ndakidemi alitoa kauli hiyo Bungeni ambapo alisema kuwa, katika hotuba ya Waziri wa Maji, Jumaa Awesso ameonyesha miaka 10 ijayo kutakuwa na upungufu wa maji kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na pia matumizi mabaya ya vyanzo vya maji.
Alisema kuwa, pia ametoa takwimu kuwa tutatumia mita za ujazo 883 badala ya 2105 ambazo zinatumika sasa hivyo inaonyesha kuwa miaka 10 inayo kutakuwa na shida ya maji na hii imeanza kujionyesha kwani kwenye manner mengi hapa nchini maji hupatikana kwa mgao na maeneo mengine hakuna.
Aliiomba Wizara kufanya kitu ambacho kitasaidia kutatua tatizo hilo kwani wasipofanya hivyo watakuwa hawajalitendea haki Taifa.
"Nitoe ushauri kwa Serikali kuja na mpango kazi wa maji wa Taifa badala ya mikoa mitatu waliyoitaja ya Dodoma, Njombe na Rukwa kwa sababu tatizo hili ni la kitaifa hivyo washirikishe mikoa yote kujua vyanzo vya maji viko wapi kwa kutumia teknolojia na kujua maji yatapatikana wapi" Alisema Prof. Ndakidemi.
Na kuongeza " Pia kujua mahitaji halisi ya maji na pia kujua makisio ya fedha ya siku zajazo na kuja na mkakati wa kutunza vyanzo ili shida itakayokuja miaka 10 ijayo tuanze kushughulikia sasa ".
Aliitaka Wizara kuishirikisha jamii kutengeneza mpango kazi huo wa maji ili jamii iwe sehemu ya hiyo na isije kuleta fujo ya kusema chanzo hiki ni mali yao.
Mbunge huyo aliitaka Serikali kuja na maoteo ya fedha itakayokidhi matakwa na ushauri utakaotokana na mpango kazi huo wa maji wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Ndakidemi aliishukuru Serikali kwa kutoa milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji katika kata ya Kimochi ambapo kumejengwa matanki mawili katika kijiji cha Liakombila.
Alisema kuwa, kwenye chanzo kunabomba za nchi tatu hali inayopelekea maji kutotosheleza ambapo katika vijiji vya Mdawi, Sango wananchi wapatao 14000 hawajapata maji na kuomba Wizara kutatua changamoto hiyo.
Pia alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa visima vitano na na kudai kuwa ameshaongea na Waandisi kwa ajili ya kujua visima hivo vitachimbwa sehemu gani.
Mwisho.
0 Comments