Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Singida,kimesema uchaguzi wa viongozi unaoendelea kufanyika katika majimbo yote ya mkoa huu utakwenda salama na kwamba hakuna viashiria vyovyote vya watu kupewa rushwa.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Emmanuel Jingu alisema hayo wakati wa mkutano mkuu maalum wa uchaguzi wa viongozi wa Jimbo la Singida mjini ambao ulisimamiwa na Mjumbe wa Kamati Kuuu ya Chadema, ,Patrick Ole Sosopi.
"Kama kuna mtu atakuwa anaongea kuhogwa fedha kwenye huu uchaguzi wa jimbo la Singida mjini atamuwa mwongo," alisema Jingu.
Alisema jimbo la Singida mjini limefanya vizuri katika usajili wa wanachama kidigitali ambapo wamesajiliwa zaidi 2000 na kwamba jimbo hilo linatakiwa kuwa la mfano na kiongozi wa majimbo yote.
Jingu alisema Chadema katika malengo ya kutaka kushika dola inalitegemea sana jimbo la Singida mjini kuyaongoza majimbo mengine na kuwataka wanachama kuchagua viongozi makini ambao watawasikiliza wananchi na wenye uwezo wa kupaza sauti kudai haki iliyoporwa.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA),Patrick Ole Sosopi, alisema kama kuna mwanachama ambaye ameshawishiwa kugombea uongozi kwa malengo fulani katika uchaguzi unaoendelea ndani chama hicho akizingua atatolewa mara moja.
"Aliyeshawishiwa kugombea kwa malengo ambayo yeye anayafahamu na yule aliyemshawishi tambua umepewa majukumu ya kutumikia chama hiki nenda kakitumikie na ukizingua tutakutoa," alisema.
Sosopi ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema watakaochaguliwa jukumu lao kubwa ni kuunganisha wanachama na chama kwenye mitaa,vitongozi na vijiji kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2025 ili chama kiweze kuibuka na ushindi.
0 Comments