Header Ads Widget

CWT-SUALA LA KIKOKOTOO LIMEWAFANYA WALIMU WAVUNJIKE MOYO WA KUFANYA KAZI

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 

CHAMA cha Walimu Tanzania  (CWT) kimesema suala la kikokotoo kinachoendelea kutumika sasa kimewafanya walimu wavunjike moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.


Katibu wa CWT Mkoa wa Singida, Digna Nyaki, amesema hayo jana wakati wa Mkutano Mkuu wa NOCETEC ambao ni umoja unaowajumuisha walimu na viongozi wa CWT kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha,Manyara,Dodoma na Singida ambao umefanyika mjini Singida.


Amesema NOCETEC ambao ulianzishwa 2022 ukiwa na lengo la kuwaunganisha walimu ili kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto zinazowakabili ili kutekeleza kauli mbiu ya Chama cha Walimu Tanzania inayosena wajibu na haki ina jumla wanachama 55,482.


Amesema CWT inapongeza serikali kwa jitihada zilizofanyika na ambazo zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa sekta ya elimu nchini inaimarika na elimu bora inaendelea kutolewa kwa kudhihirisha hilo ni matokeo ya kitaifa kwa ngazi zote ambapo ufaulu umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.


"CWT kwa kushirikiana na serikali tumepata mafanikio makubwa katika kuboresha maslahi ya walimu kama vile ajira mpya kwa walimu nchi nzima, nyongeza za mishahara,upandishwaji wa madaraja kwa wakimu ambayo ilikuwa kilio cha muda mrefu,stahiki za walimu kama fedha za likizo,matibabu na malimbikizo ya mishahara na fedha za wastaafu na kuimarika kwa mahusiano mazuri kati ya CWT na Serikali," amesema.


Nyaki amesema pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto  kadhaa ikiwamo kuwepo kwa upungufu mkubwa wa walimu katika shule za msingi na sekondari,walimu wengi wenye madeni bado hawajalipwa licha ya kwamba yamehakikiwa tangu 2017 na walimu waliopandishwa madaraja bado hawajapewa madaraja yanayostahili.


Amesema changamoto nyingine mchakato wa walimu waliostahili kupandishwa madaraja katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 umekuwa kimya hali inayotia wasiwasi kwa walimu na pia mabadiliko ya mtaala bado hakuna vifaa vya kufundishia hasa vitabu vya kinda na ziada hali inayowafanya walimu kutofundisha kwa ufanisi.


Nyaki alieleza changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya viongozi ngazi ya wilaya kutowasikiliza na kuwahudumia walimu ipasavyo pale wanapopeleka changamoto zao kwenye ofisi zao na pia Mfuko wa Bima uangaliwe upya kwani umekuwa mwiba kwa watumishi na wategemezi kufuatia kuondolewa katika kitita cha awali.


Aidha, amesema suala la kikokotoo kinachoendelea kutumika sasa kimewafanya walimu wavunjike moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.



Naye Mwenyekiti  wa CWT Mkoa wa Singida  ambaye pia ni Mwenyeki wa NOCETEC Kanda ya Kati na Kaskazini, Hamisi Mtundua, amesema iharakishe mchakato wa kutoa waraka wa kupandishwa vyeo watumishi ambao umechelewa kutolewa kwani kwa mujibu wa taratibu vyeo vya watumishi vinapaswa kupanda kuanzia Julai Mosi mwaka huu.


"Walimu hawa ili waendelee kuwa na nyuso za furaha ni lazima wapewe kile wanachostahili kukipata,mpaka sasa tulitakiwa tuwe tumepewa waraka wa kupandishwa vyeo lakini hadi sasa hatujapata na kwa mujibu wa taratibu cheo kinapaswa kupanda Julai Mosi lakini tumecheleweshewa," amesema Mtundua na kushangiliwa na mamia ya walimu wanaohudhuria mkutano huo.


Mtundua ambaye pia Mwenyekiti  wa CWT Mkoa wa Singida, amesema suala la kikokotoo bado walimu hawajamalizana na serikali na kwamba bado wana imani kubwa na serikali italifanyia kazi suala hilo kwani kile wanachokipata walimu hakitoshelezi kabisa.


RAIS  WA CWT AELEZA WAJIBU NA HAKI

Naye Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Leah Ulaya, amesema walimu wana kauli mbiu yao inayoitwa wajibu na haki ambayo ili waweze kutimiza wajibu wao ni lazima kuwa na viongozi mahili.


" Ili tuweze kutimiza wajibu wetu kuna mambo matatu ya kuzingatia ambayo ni, mosi, kuwe na uhusiano wa kati ya pande mbili yaani mwajiri na mwajiriwa na yawe mahusiano mazuri ambayo yatafanya daraja kati ya mwajiriwa na Afisa Utumishi," amesema Ulaya.


Ulaya ameongeza jambo jingine la pili ili walimu waweze kutimiza wajibu wao kama watumishi wa umma ni lazima kuwa na uzalendo,uzalendo ambao unashehenezwa na upendo na kiongozi anayetusimamia.


" Ni dhahiri sana walimu tunahitaji kushikwa na kukumbatiwa kwani mwalimu ni daktari,polisi,msuluhishi mwana saikolojia,mzazi,mlezi,mkulima,mwalimu ni kila kitu katika maisha ya jamii,kwa maana hiyo mwalimu anatakiwa kuangaliwa kwa jicho la kipekee sana," amesema.


Rais huyo wa CWT ameongeza kuwa walimu wanatamani kuona yale mambo yao yote wanayohitaji kuyapata wayapate kwa wakati na pia wanatamini kuona mshikamano baina yao na serikali.

RC DENDEGO-WATUMISHI MAOFISINI ACHENI URASIMU


Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego, amewagiza wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya wasirundike matatizo yanayowakabili watumishi badala yake wayatafutie ufumbuzi haraka.


"Tuache urasimu katika mambo yanayohusu maslahi ya watu,nawaagiza Ma-DED mhamikishe madai yote ya watumishi wakiwamo walimu yanafanyiwa kazi,"amesema.


Aidha, Dendego amesisitiza suala la kuwadhibu wanafunzi wanapofanya makosa na kwamba kwa walimu aliyopo Mkoa wa Singida kama kuna mzazi ambaye atakuja juu kisa mtoto wake amepigwa viboko atoe taarifa.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI