Na Fredrick Siwale - Matukio Daima APP Mafinga.
AGIZO la Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh.Peter Serukamba la kuagiza kuvunjwa kwa soko kuu Mafinga wilaya ya Mufindi mkoani Iringa limeanza kutekelezwa kwa kufunga utepe wa zuio la biashara kuendelea kufanyika sokoni hapo.
Amri na maagizo hayo yametolewa na Mh.Serukamba kwenye kikao cha kawaida cha robo ya tatu ya baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Mafinga kufuatia kuwepo kwa mgogoro wa vibanda 331 vinavyodaiwa kujengwa na Wafanyabiashara hao ambavyo Serikali iliagiza waingie mkataba wa miaka 14 ili wa Wafanyabiashara hao wawe wapangaji badala ya Wamiliki.
Baada ya tamko la awali kutolewa na Serikali na kutolewa kwa muda wa kuingia mikataba wafanyabiashara inadaiwa kuwa hawakuafiki na kuhitaji makubaliano ambayo yalishindikana na Halmashauri kutoa siku 21 ili kuruhusu Wafanyabiashara kuondoa bidhaa zao na kuvunja vibada ili kuruhusu Halmashauri kupanga matumizi ya Ardhi yao.
" Naagiza kufungwa utepe na kesho Jumanne Mkurugenzi peleka greda na kuanza zoezi la ubomoaji bila kuchelewa."Alisema RC Serukamba.
Baada ya maagizo hayo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji Mafinga Fedelica Myovella alituma tume ya Watumishi wakiongozwa afisa biashara Evance na mwanasheria wa Halmashauri ya Mafinga Mji wameanza kufunga utepe kuashiria kutekelezeka kwa agizo la Mkuu wa Mkoa.
Hadi habari hii inatumwa Wamiliki wa Vimbanda 331 pamoja na baadhi ya Wafanyabiasha katika Soko hilo wameonekana wakielekea maeneo tofauti tofauti kukaa vikao vyao vya siri ili kujaribu kuona jinsi ya kujinasua na utekelezwaji wa maagizo ya Mkuu wa mkoa la kutakiwa kuondoa bidhaa zao na wakiweza kuvunja Vibanda vyao kabla ya zoezi la uvunjaji kuanza kutekelezwa mei 21 mwaka huu 2024.
Mwisho
0 Comments