Header Ads Widget

ZAO LA TUMBAKU LAIINGIZIA TAIFA MAPATO YA FEDHA ZA KIGENI DOLA MIL.394

 


Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA


ZAO la Tumbaku ambalo katika msimu wa 2022/2023 limeshika nafasi ya kwanza katika kuliingizia taifa mapato ya fedha za kigeni hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu limeingiza Dola za Marekani milioni 394.


Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku  Tanzania,Stanley Mnozya, amesema hayo leo (April 17, 2024) wakati wa mkutano wa mwaka 2024 ambao unawashirikisha washiriki kutoka mikoa inayozalisha tumbaku ambayo ni Iringa,Ruvuma,Katavi,Tabora,Kigoma,Shinyanga,Singida,Mara,Geita,Kagera,Morogoro  na Mbeya.


Alisema zao la Tumbaku lina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchini ambapo kutokana umuhimu huo mkubwa uliifanya serikali kutoa agizo la kuongezwa kwa uzalishaji wa zao hilo hadi kufikia kilo 200,000,000 ifikapo mwaka 2025.


Mnozya alisema hivi sasa mapato ya wakulima yameongezeka kutoka Sh.121,582,427,500 mwaka 2021/2022  hadi kufikia Sh. 401,538,833,087 mwaka 2022/2023 sawa na ongezekobla asilimia 230.


Amesema mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuongezeka kwa makusanyo ya ushuru wa Halmashauri za Wilaya kutoka Sh.bilioni 7.5 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh.bilioni 21.5 mwaka 2022/2023  sawa na ongezeko la asilimia 186.6.


Ameongeza kuwa mapato ya fedha za kigeni yameongezeka kutoka Dola za Marekani  186,639,238.57 mwaka 2022/2023 hadi kufikia dola 394,452,618 15 mwaka 2023/2024  sawa na ongezeko la asilimia 112.5 ambayo ni kulingana na ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Machi 2024.


Mnozya ameongeza kuwa mafanikio mengine yaliyopatikana kutoka na zao la Tumbaku ni limechangia mapato  zaidi ya Dola za Marekani 696,599,513 wenye uchumi wa nchi kutokana na makusanyo mbalimbali ya zao kufikia Machi 2024 na ifikapo Juni 2024 litachangia mapato dola milioni 762.


Mkurugenzi huyo amesema uzalishaji wa tumbaku umekuwa ukiongezeka ambapo katika msimu wa 2020/2021 zilizalishwa kilo 58,507,937, msimu wa 2021/2022 kilo 60,874,831, msimubwa 2022/2023 kilo 122,858,564 na msimu wa 2023/2024 kuna matarajio ya kuzalisha kilo 178,521,508.


Amesema makampuni ya ununuzi yameongezeka kutoka matatu katika msimubwa 2019/2020 na kufikia matano  na msimu wa 2023/2024  yapo 12 jambo ambalo litaongeza ushindani na kuleta uhakika wa soko kwa wakulima wa tumbaku.


Kuhusu bei ya tumbaku, Mkurugenzi huyo amesema imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka mfano msimu wa 2020/2021 tumbaku ya mvuke ilikuwa Dola za Marekani 1.62 hadi kufikia wastani wa dola 2.33 msimu wa 2022/2023 huku daraja la kwanza likiwa na bei ya Dola 3.2 kwa kilo moja.


Amesema pamoja na mafanikio hayo sekta ndogo ya tumbaku imekuwa na changamoto kadhaa ikiwamo kuchelewa kwa mbolea,mabadiliko ya tabia ya nchi na hali ya hewa ambayo inasababisha ukame na tija ndogo ya uzalishaji ambapo wakulima hawazalishi tumbaku kwa kiwango ambacho kinaendana na gharama za uzalishaji.


Mnozya amesema katika kuifanya tasnia ya tumbaku inakuwa endelevu na yenye mchango kwa maendeleo ya taifa, Bodi ya Tumbaku Tanzania inatarajia kuhakikisha uzalishaji unaongezeka hadi kufikia kilo 200,000 ifikapo 2025 kuogeza tija ya uzalishaji kutoka kilo 1,300 kwa hekta hadi kufikia 1,750 kwa heka.


Mipango mingine ni kuongeza ujenzi wa mabani ya kisasa na majiko sanifu ambayo yanatumia kuni chache na kutoa tumbaku zenye ubora,kusimamia matumizi ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) TEHAMA  na mifumo ya mawasiliano hasa kwa Bodi ya Tumbaku,Vyama vya Msingi na Tume ya Maendeleo ya Ushirika ili kurahisisha utendaji wa shughuli za kila siku.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida,Godwin Gondwe ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego, amesema serikali inatambua umuhimu wa zao la Tumbaku katika kukuza pato la taifa.


Amesema kwa kuzingatia kuwa zaidia ya asilimia 70 ya watanzania wanategemea kilimo na kilimo ni uti wa mgongo kuna umuhimu wa kuwekeza katika mazao ya biashara pamoja na mazao ya chakula ili kuimarisha uchumi wetu.


"Serikali inajivunia mafanikio makubwa katika kilimo cha tumbaku ndani ya kipindi hiki kifupi cha miaka miwili baada ya kupita katika mdororo  wa miaka kadhaa hapo nyuma,"amesema Gondwe.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS