Header Ads Widget

MAENDELEO YA NCHI NI KUWA NA USALAMA WA CHAKULA

 








Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma


WAZIRI wa Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo amesema Hatua ya kwanza kujipima katika maendeleo ni kuwa na usalama wa chakula katika nchi. 


Hayo ameyasema leo jijini Dodoma alipokuwa kwenye mkutano na waandishi wa Habari na kuelezea kuhusu mafanikio ya miaka 60 ndani ya Wizara hiyo ya Mipango na Uwekezaji. 


Amesema kipinda Tanganyika na Zanzibar tumeungana, usalama wa chakula ulikuwa asilimia 60 huku lengo la nchi ni kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100 na kuwa na akiba. 


" Ila kwa sasa tumepiga hatua kubwa ambapo kwa sasa nchi ina usalama wa chakula kwa asilimia 124," Amesema Prof.Mkumbo


Aidha Prof Mkumbo amesema Hatua ya pili kujipima katika maendeleo ni ustawi wa watu na nchi kwa kuangalia mambo ya msingi ya kibinadamu ikiwemo chakula, mavazi na malazi ambayo nayo tumepiga hatua kubwa.


"Wakati tunapata Uhuru, umri wa kuishi kwa Mtanzania ilikuwa wastani wa miaka 32, mwaka 2000 umri wa kuishi ukasogea hadi wastani wa miaka 52," 



Na kuongeza "Tamaa yetu ifikapo mwaka kesho 2025 wastani wa kuishi uwe miaka 68. Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, wastani wa kuishi ni miaka 66," Amesema Prof Mkumbo.


Hata hivyo amebainisha kuwa Mambo matatu ya kufanya kukuza ustawi wa binadamu ni kumpa binadamu elimu ili aweze kuishi vizuri ambapo mwaka 2000 nchini Tanzania, kiwango cha kuandikisha wanafunzi kilikuwa asilimia 69. 


Amesema Kwa malengo tuliyojiwekea kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, ni kufikia asilimia 100 ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo hadi sasa tumevuka malengo, tupo asilimia 108.5.


Kuhusu suala la kwenda sekondari,amesema  mnamo mwaka 1964 ilikuwa asilimia 5, mnamo mwaka 2000, watoto waliofanikiwa kufika sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa chini ya asilimia 20 . 


"Lengo letu ifikapo mwaka 2025, tuwe tumefika asilimia 48. Kwa takwimu za hivi sasa, tupo asilimia 70," Amesema .


Sambamba na hilo ameeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa inayokuja, tutahitaji elimu ya msingi Tanzania iwe kwa Watanzania wote na wote lazima kufika sekondari kwa asilimia 100.


Amesema Eneo la pili la kukuza ustawi wa binadamu ni afya hasa kwenye eneo la mama na mtoto, na la tatu ni maji ambapo wakati tunapata uhuru, uwepo wa maji vijijini ulikuwa chini ya asilimia 15 na mwaka 2000 ilikuwa asilimia 32. Kwa sasa ni asilimia 77.


"Nchi inahitaji uwepo wa uchumi, kukua kwa uchumi ni nyenzo muhimu. Ili nchi ione inapiga hatua ni lazima iangalie uchumi unaendaje. Wakati wa Uhuru ilikuwa ni kilimo peke yake, lakini katika miaka takriban 20 iliyopita, uchumi wetu umekuwa ukikua vizuri kati ya wastani wa asilimia 6 mpaka 7.," Amesema


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS