NA HADIJA OMARY - LINDI.
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa kifuta jasho na kifuta machozi cha zaidi ya shillingi millioni 399 kwa wananchi 1,658 walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 09, 2024 na Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mhe. Mohamed Hassan Moyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
Moyo alisema Serikali kupitia utaratibu wake wa kifuta jasho na kifuta machozi, imewapatia fidia wahanga zaidi ya 1658 kwenye wilaya hiyo, ambao walipata maafa ya wanyama wakali kwa mwaka 2023
Na kuongeza kuwa serikali ilitoa fedha kwa ajili ya wananchi walioathiriwa na wanyama hao na kufanyiwa tathmini mwaka 2021/2022 walilipwa fedha zao kiasi cha shilingi 399, 405,000/=
Hata hivyo Moyo alisema wilaya yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo wanaoathiri mali na maisha ya wananchi lakini pamoja na changamoto hizo amekiri kuwepo na jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA na TAWIRI katika kuelimisha wananchi mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori pamoja na kuwadhibiti.
Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni Kanda ya Kusini Mashariki Linus Chuwa amesema katika kuendeleza jitihada za kukabiliana na wanyama hao wakali na waharibifu TAWA imeanzisha vituo 10 vya Askari wa kukabiliana na wanyamapori hao ambapo vitano kati ya 10 ni vya kudumu na vingine vitano ni vya muda mfupi hasa pale matukio ya wanyamapori hao yanapojitokeza.
Amesema TAWA pia imefanikiwa kununua gari jipya katika kituo cha malola ambalo hutumiwa na Askari wa kituo hicho, pia imenunua ndege nyuki (drones) maalumu kwa ajili ya kufukuzia tembo ambazo zilitumika katika zoezi la kufukuza tembo mwaka jana (2023), zoezi ambalo linatajwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Jitihada zingine zilizofanywa na TAWA kwa kushirikiana na wadau ni pamoja na kuwafunga visukuma mawimbi tembo watatu ambao ni viongozi wa makundi na hivyo kufuatilia mienendo yao ili kuwadhibiti kabla hawajafika katika makazi ya binadamu.
Mhifadhi Mkuu Linus Chuwa ameongeza kusema TAWA imepeleka Askari wa wanyamapori wa vijiji 41 (VGS) katika chuo cha Likuyu Sekamaganga kwa ajili ya kupatiwa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na amethibitisha kuwa Askari hao hutumiwa na TAWA Katika matukio mbalimbali ya kudhibiti wanyamapori hao
Kwa upande wake, Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja amesema lengo kuu la ziara hiyo Mkoani humo ni kuelezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA Katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu na kuwahakikishia wananchi kuwa TAWA iko kazini kuhakikisha inafanya Kila iwezalo kuwadhibiti wanyamapori hao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile TAWIRI, GIZ na TANAPA.
Mwisho
0 Comments