Bei ya hisa za kampuni ya habari ya Donald Trump imeshuka kwa kiwango kukubwa wiki iliyopita ilipoorodheshwa rasmi kwenye soko la hisa la Nasdaq.
Lakini bado ina thamani ya zaidi ya dola bilioni saba kwa bei za sasa - kiasi cha kushangaza kutokana na biashara iliyoifanya.
Mtandao wa Truth Social ni nini, unamilikiwa na nani, una watumiaji wangapi, na unatengeneza pesa kiwango gani? Na Je, ni jibu kwa gharama kubwa ya kisheria ya Bw Tru
Trump Media na Truth Social ni nini?
Trump Media & Technology Group ilianzishwa mwaka wa 2021 baada ya Bw Trump kushindwa katika uchaguzi wa urais na akatolewa kwa muda kutoka kwa mitandao mikuu ya kijamii, ikiwemo Twitter na Facebook, ambayo ilimshutumu kwa kuchochea ghasia.
Wazo hilo lilitolewa kwake na wanaume wawili, washindani wa zamani kwenye kipindi chake cha Televisheni, The Apprentice, ambao waliona fursa ya kuunda njia mbadala ya tovuti kuu za mitandao ya kijamii.
Mnamo 2022 Trump Media ilizindua bidhaa yake ya kwanza na ya pekee hadi sasa kwa umma: mtandao wa kijamii Truth Social.
Utendakazi mwingi wa Truth Social unafanana na X. Watumiaji wanaweza kuchapisha 'truths' au 'retruths' na pia kutuma ujumbe wa moja kwa moja. Matangazo huwa yanaitwa 'sponsored truths'.
Una watumiaji wangapi?
Trump Media inasema takriban akaunti milioni 9 zimeundwa tangu kuanza kwake.
Haifichui ina watumiaji wangapi, lakini kampuni ya utafiti ya SimilarWeb inakadiria kuwa Truth Social ilitembelewa mara milioni 5 mwezi Februari mwaka huu.
Kwa kulinganisha, TikTok ilitembelewa zaidi ya mara bilioni 2, wakati Facebook ikitembelewa zaidi ya mara bilioni 3. X ilitembelewa zaidi ya mara milioni 104 mnamo Februari, kulingana na SimilarWeb.
Bw Trump ana takriban wafuasi milioni 7 kwenye Truth Social, wachache zaidi ya milioni 87 alionao kwenye X. Akaunti ya X ya rais huyo wa zamani ilirejeshwa mwishoni mwa 2022, lakini amechapisha mara moja tu tangu wakati huo.
Inatengeneza pesa ngapi?
Haitengenezi.
Trump Media ilipoteza karibu dola milioni 60 mnamo 2023, huku ikileta mapato ya takriban dola milioni 4 tu kutoka kwa matangazo, kulingana na sasisho lake la hivi karibuni la kifedha, ambalo pia lilionya juu ya "mashaka makubwa" juu ya uwezo wake wa kuendelea kama biashara.
Ripoti hiyo ilikuwa ukumbusho mwingine wa ukosefu wa uhusiano kati ya fedha za kampuni na bei yake ya hisa, ambayo inaweka thamani yake kuwa karibu dola bilioni 7.
Kama kipimo, mnamo 2013, Twitter ilipoorodheshwa kwenye soko la hisa, iliripoti mapato ya dola milioni 660 na ilikuwa na thamani ya soko ya takriban dola bilioni 24.
Kufikia 2021, mwaka mmoja kabla ya Elon Musk kununua Twitter kwa dola bilioni 44, kiwango hicho kilikuwa kimeongezeka hadi zaidi ya dola bilioni 5.
Trump anafanya nini kwenye kampuni?
Uhusiano wa Bw Trump na kampuni hiyo ni sawa na mikataba ya leseni ambayo alitumia katika himaya yake ya mali, ambapo alitia saini kupitia jina lake ili kukuza biashara inayoendeshwa na watu wengine.
Katika hali hii, Bw Trump pia amekubali kutuma jumbe zisizo za kisiasa kwanza kwenye Truth Social.
Tofauti nyingine ni kwamba mkataba huu haukuzaa ada za leseni badala yake, Bw Trump alilipwa kwa kupewa hisa katika kampuni hiyo mpya.
Kwa hivyo mmiliki ni nani?
Trump Media, ambayo inaongozwa na mbunge wa zamani wa chama cha Republican Devin Nunes, awali ilikuwa kampuni ya kibinafsi, na Bw Trump alimiliki asilimia 90 ya kampuni.
Iliorodheshwa kwa soko la hisa Machi 2024 kupitia kile kinachojulikana kama SPAC - kimsingi, ilinunuliwa na kampuni ambayo hisa zake tayari zilikuwa zikifanya biashara kwenye soko la hisa, au Digital World Acquisition Corp.
Bw Trump sasa anamiliki takriban asilimia 57 ya hisa katika kampuni hiyo iliyounganishwa, ambayo ilipewa jina la Trump Media na inafanya biashara kama DJT - herufi za kwanza za Bw Trump.mp?
Mmiliki mkuu anayefuata wa TMTG ni kampuni ya uwekezaji yenye makao yake makuu ya Kuwait ya ARC Global Investments, ambayo ina asilimi 6.9, kulingana na ripoti za Trump Media na wadhibiti wa kifedha.
Washiriki wa zamani wa Apprentice pia wana hisa kubwa, ingawa umiliki huo kwa sasa unakabiliwa na mizozano ya kisheria.
Nani mwingine anamiliki hisa?
Wakati Trump Media ilipotangaza mipango yake ya kuingia soko la hisa mnamo 2021, taarifa hiyo iliwafanya wawekezaji wa muda kununua hisa za Digital World, na kusaidia kuongeza bei yake na kulinganisha na hisa za wakati wa janga.
Mwishoni mwa 2023, makampuni makubwa ya kifedha yalimiliki takriban asilimia 5 tu ya hisa ya Digital World, chini sana kuliko ilivyo kawaida, ikimaanisha kuwa wawekezaji wa kila siku walikuwa na sehemu kubwa ya iliyobaki.
Pamoja na muunganisho kukamilika, watu hao sasa pia wanamiliki sehemu kubwa ya Trump Media, ingawa haijulikani ni kiasi gani haswa.
Mazungumzo katika vikao vya mtandaoni yanapendekeza angalau baadhi ya wanahisa hao kuona ununuzi wao wa hisa kama dau kwa Bw Trump na njia ya kumuunga mkono kwani matatizo yake ya kisheria, na bili zinazoandamana nao, zikirundikana.
Bw Trump ameagizwa kulipa fidia ya zaidi ya dola milioni 350 katika kesi ya ulaghai, huku tozo za riba zikiongeza dola milioni 100 zaidi.
Hii itasuluhisha shida za kifedha za Donald Trump?
Baada ya muungano kukamilika, Bw Trump aliona utajiri wake ukiwa na thamani ya zaidi ya mara mbili hadi zaidi ya dola bilioni 5 kwa usiku mmoja, kulingana na Forbes.
Bw Trump hataruhusiwa kuuza hisa zake takriban milioni 78 kwa miezi sita, isipokuwa kampuni hiyo itaamua kumpa msamaha.
Lakini ana fursa ya kupata matokeo mazuri ikiwa ataamua kuingiza pesa - hata kama bei itashuka sana, kama wachambuzi wengi wanavyotabiri.
Hisa katika Digital World, ambayo sasa ni Trump Media, zimeyumba sana tangu 2021 na zinatarajiwa kuendelea kufanya hivyo.
Zilipanda hadi zaidi ya dola 70 kila moja wakati Trump Media ilipoanza rasmi tarehe 26 Machi.
Tangu wakati huo zimeshuka na sasa zinauzwa kwa karibu dola 50 kila mmoja, jambo ambalo linafanya hisa za Bw Trump kuwa na thamani ya dola bilioni 4.1.
Lakini hiyo ni kuhusu pale zilipokuwa siku moja kabla ya uzinduzi na mara tatu ya thamani ya hisa za Digital World mwanzoni mwa 2024.
Hata kama zitapungua hadi dola 1 kila baada ya miezi sita, Bw Trump bado anaweza kupata zaidi ya dola milioni 78 kwa kuuza.
0 Comments