NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Godfrey Mzava alisema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa kituo hicho kwani umezingatia thamani ya fedha.
Mzava alisema kuwa, lengo la serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya Afya karibu na kuwapongeza wananchi wa Ushirika katika kata ya Uru kusini kutoa eneo ambalo kituo hicho kimejengwa pamoja na kuanza ujenzi kwa nguvu zao.
"Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuboresha sekta ya Afya ambapo tumeshuhudia hospitali za wilaya, mikoa, vituo vya Afya na hata zahanati zikijengwa kwa wingi katika kipindi chake na vifaa tiba vikiwekwa" Alisema Mzava.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi alisema kuwa, Jimbo hilo limepokea fedha nyingi za maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita.
Prof. Ndakidemi alisema kuwa, miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni pamoja na kituo hicho cha Afya, hospitali ya wilaya, miradi ya maji, barabara na kwenye sekta ya elimu.
"Hawa wananchi wa kata ya Uru kusini walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Afya lakini kukamilika kwa kituo hiki umewarahisishia kupata huduma karibu zaidi" Alisema Prof. Ndakidemi.
Naye Diwani wa kata ya Uru kusini, Wilhard Kitale alisema kuwa, wananchi walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 5 mpaka nane kufuata huduma za afya lakini kukamilika kwako kutaondoa hadha ya kutembea umbali huo.
Alitumia nafasi hiyo kuishukuru serikali kwa kuwajengea kituo hicho pamoja na wananchi ambao walijitolea nguvu kazi zao pamoja na eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Miradi mingine iliyotembelewa ni mradi wa kiwanda cha mvinyo Classic Bevarage masters kilichopo kata ya Kimochi ambapo mwenge wa uhuru ulikizindua, pamoja na kutembelea eneo la mradi wa kitalu nyumba cha mafunzo ya kilimo kwa kikundi cha vijana KDC.
Mwisho...
0 Comments