WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo Dkt Charles Stephen Kimei amekabidhi tende boksi 35 kwa viongozi wa BAKWATA wilaya Hussein Jamal na Katibu wake pamoja na maimamu wa misikiti iliyopo katika kata 16 za Jimbo la Vunjo.
Katika hafla hiyo alishiriki pia Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephania Sumaye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Shadrack Mhagama pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya Shabani Mchomvu.
Akikabidhi tende hizo Dkt Kimei amesema Tende ni tunda tamu lenye thamani ya lishe na kimatibabu hivyo kupendwa kutumiwa na watu wengi kote duniani.
Pia amesisitiza tende ni maarufu miongoni mwa Waislamu hasa wakati wa Ramadhani kwani zimeorodheshwa miongoni mwa matunda yaliyobarikiwa Peponi.
Dkt Kimei amesisitiza hata Mtume Muhammad (SAW) aliwahimiza Waislamu kufungua swaumu yao kwa kutumia tende na ndiyo maana hata moja kati ya masomo ya Kiislamu kupitia Hadithi inasema Mtu anapofungua swaumu yake, na afungue na tende kwani zimebarikiwa.
"Ikiwa hazipatikani, na afungue kwa maji kwani ni safi niwaombe waumini wa Kiislamu kuendelea kuiombea nchi yetu amani, usalama dhidi ya majanga mbalimbali pamoja na kumuombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuiongoza nchi yetu katika haki na ustawi wa wananchi wote" Alisema Dkt Kimei.
Zoezi hilo ni muendelezo wa utaratibu aliojiwekea tangu ameingia madarakani katika kutoa sadaka ya futari kuwaunga mkono waumini wa dini ya kiislamu waliofunga mwezi mtukufu wa Ramadhan moja kati ya nguzo muhimu katika imani yao.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Moshi Sumaye amempongeza Mbunge Dkt Kimei kwa mshikamano huo aliouonesha kwa waumini wa dini ya Kiislamu kwa kuwaunga mkono katika kutekeleza ibada ya funga katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Naye Hussein Jamal kwa niaba ya uongozi wa BAKWATA wilaya na viongozi wote wa misikiti amemshukuru Mbunge Dkt Kimei kwa sadaka ya tende aliyoitoa ambayo hawana cha kumlipa zaidi ya kumuombea afya njema kwake binafsi na familia yake pamoja na mafanikio katika majukumu yake.
Mwisho..
0 Comments