NaMwanahabari wetu, Matukio Daima App,
Imedhibitishwa kuwa Biashara na matumizi ya madawa ya kulevya ni moja ya matishio makubwa kiusalama Duniani hasa ikizingatiwa kuwa, Vijana ndio kundi kubwa linaloathiriwa zaidi na dawa hizo.
Kwa Mujibu wa Takwimu ya Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022, imeweka wazi kuwa idadi ya Vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa ni 20, 612, 560 ni sawa na wastani wa 50% ya idadi ya watu wote nchini Tanzania.
Kati ya Watuhumiwa wanaokamatwa, wengi wao wako katika kundi la Vijana, ikiwa kundi hili litaendelea litaachwa kwenye biashara na matumizi ya dawa za kulevya tutapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa na hatimaye kuhatarisha uchumi na usalama wa Taifa.
Serikali ya awamu ya sita imekuja na mpango madhubuti wa kuhakikisha unainusulu idadi kubwa ya vijana walio kwenye hatari ya kuingia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa kuandaa sera madhubuti na mfumo wa kupambana na kuzuia uingizwaji wa madawa hayo ya kulevya.
Ni ukweli kabisa usiopingika Tanzania bila matumizi ya dawa za kulevya inawezekana! Ndio inawezekana kabisa iwapo kila mmoja wetu akiamua kushiriki kikamilifu kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Tunafahamu taasisi mbalimbali za umma na binafsi ambavyo zinashirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA) nchini katika kuhakikisha biashara ya dawa hizo inakoma, Kwa sehemu kubwa ushirikiano huo umekuwa ukisaidia katika mapambano ya dawa za kulevya.
Hata hivyo katika kukomesha biashara ya dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mbali ya kushirikiana na wadau wengine, yenyewe imekuwa na mikakati madhubuti wanayoitumia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, iwe usiku, iwe mchana, iwe asubuhi, iwe jioni.
Kwa kudhibitisha hilo Kamishna Jenerali Lyimo anajitokeza mbele ya Vyombo vya Habari na kuueleza Umma kuwa Mamlaka hiyo ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za Kulevya (DCEA), pamoja na wananchi wanawajibu wa kushiriki katika vita dhidi ya Biashara na Matumizi ya madawa ya kulevya.
Ameyasema hayo alipokuwa akitoa ripoti ya operesheni iliyofanikiwa kukamata jumla ya kiligramu 767.2, za dawa za kulevya katika operesheni iliyofanyika katika Mikoa ya Dar es salaam, Tanga na Pwani kuanzia tarehe 4 hadi 18 aprili 2024.
Katika operesheni hiyo kati ya dawa zilizokamatwa, kilogramu 233.2, ni heroin, kilogramu 525.67 ni Methamphetamine na kilogramu 8.33 ya Skanka, na jumla ya Watuhumiwa 21, walikamatwa kuhusika na dawa hizo za kulevya, baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa taratibu za kisheria zitakavyo kamilika.
Anasema kuwa "Operesheni zilizofanikiwa katika ukamataji huu ni kama: Tarehe 04 Aprili 2024, katika eneo la Mikwajuni Jijini Tanga, watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya Heroin kiasi cha kilogramu 329.412, na tarehe 08 aprili 2024, eneo la Wailes Temeke mtaa wa Jeshini Jijini Dar es salaam zilikamatwa kilogramu 1.48 za dawa za kulevya aina ya Skanka ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa kuhusika na dawa hizo".
Aidha Kamishna anafafanua kuwa katika operesheni iliyofanyika tarehe 10 aprili, eneo la Zinga Bagamoyo Mkoani Pwani, zilikamatwa kilogramu 424.84, za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine, na jumla ya watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusika na dawa hizo, na tarehe hiyo hiyo katika eneo la Kunduchi Jijini Dar es salaam, alikamatwa Mtuhumiwa mmoja akiwa na dawa za kulevya aina ya Heroin kiasi cha gramu 158.24.
"Tarehe 14Aprili 2024 eneo la Bandari Jijini Dar es salaam, zilikamatwa jumla ya kilogramu 4.72, za dawa za kulevya aina ya Skanka na watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusika na dawa hizo, aidha tarehe 16 aprili 2024 katika Kata ya Kunduchi Jijini Dar es salaam zilikamatwa kilogramu 232.69 za dawa za kulevya aina ya heroin na kilogramu 100.83 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi" alisema Kamishna.
Pia amesema kuwa tarehe 18 aprili 2024, mtuhumiwa mmoja alikamatwa eneo la Bandari Jijini Dar es salaam akiwa na kilogramu 2.12 za Skanka.
Hata hivyo Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Madawa ya kulevya imetoa shukrani kwa wadau wote wakiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Mamlaka kwa namna moja ama nyingine kufanikisha mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, pia wananchi wametakiwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya kwa kupiga namba 119.
0 Comments