Header Ads Widget

DC KASILDA MGENI AWAONYA WANANCHI WAPOTOSHAJI..

 


NA WILLIUM PAUL, SAME. 



MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amewaonya wananchi Wilayani humo kuacha tabia ya kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo ambazo zinazua taharuki  juu ya mambo mbalimbali ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali.



Kauli hiyo inakuja baada ya siku chache kuibuka baadhi ya watu na kusambaza taarifa kuhusu kuliwa kwa fedha milioni 500 ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha Afya Ruvu kilichopo Kata ya Ruvu wakidai kuwa hakuna kituo cha Afya kilichojengwa eneo hilo.


Kufuatia sintofahamu hiyo Mkuu wa Wilaya Kasilda Mgeni amefika  kwenye kituo hicho kukagua hali ya utekelezaji wa miradi pamoja na kufanya mkutano na wananchi ambapo amesisitiza wananchi kuwa kila mmoja anawajibu wa kufuatilia na kuhoji kujua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye jamii yake na siyo kupotosha umma kwa kutoa taarifa zisizo sahihi ambazo zinapelekea kuzua taharuki.



"Nimefanya ziara kata ya Ruvu kwenye kituo cha Afya kujionea hali ya utekelezaji wa mradi, maagizo yangu kwa Halmashauri ya Same nawapa mwezi mmoja kuhakikisha mkandarasi anasimamiwa kikamilifu na mradi uwe umekamilika, ili wananchi waweze kunufaika na fedha zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" alisema Kasilda



Aidha ujenzi wa mradi huo uliibuliwa na wananchi kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kukosa huduma ya Afya karibu, hivyo kupelekea Halmashauri mnamo Machi 30, 2022 kuanza utekelezaji wake kupitia fedha za Tozo na Serikali kuu na kufikia June 06, 2022 Mwenge wa Uhuru kitaifa kutembelea ujenzi na kuweka jiwe la msingi.



Kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo utagharimu Serikali kiasi cha  milioni 840, 000, 000 ambapo kati yake fedha milioni 600, 000, 000 kwa ajili ya ujenzi na milioni 240, 000, 000 kwa ajili ya vifaa tiba, na kinatarajiwa kunufaisha wananchi zaidi ya 13,400 wa kata ya Ruvu na maeneo jirani ya Simanjiro ambao walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilomita 30 kufuata huduma ya Afya Hospitali ya Wilaya ya Same.


Pia ujenzi huo unajumuisha majengo saba ya kutolea huduma ambayo ni Jengo la maabara, Upasuaji, Kichomea taka, choo, Jengo la mama na mtoto, wagonjwa wa nje na Jengo la kufulia nguo, hivyo kufanya Wilaya ya Same kuwa na vituo vya Afya 9 kutoka 6 vilivyokuwepo mwaka 2021/22.



Mwisho.. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS