Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda,amesema kuna tafiti zinaendelea kufanywa na wataalam kuhusu sumu ya nyuki ambayo inauzwa kwa Sh.milionin150 kwa kilo na kuna matumaini makubwa kwamba itaweza kutumika kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa kansa na ukimwi.
Alisema hayo juzi wakati akifungua mkutano mkuu wa wafugaji wa nyuki wa Mkoa wa Singida ulioandaliwa na kampuni ya Kijiji Cha Nyuki Co. Ltd, ambao pamoja na mambo mengine wafugaji walipitisha rasimu ya mwisho ya kuundwa kwa Umoja wa Wadau wa Nyuki Mkoa wa Singida na kugawiwa mavazi ya nyuki na kifaa cha kuvuna vumbi la Singida.
"Chanzo cha sumu ya nyuki kuuzwa ghari ni kwamba kuna tafiti zinaendelea na zinaweza kuleta matunda itatibu kama sio kumaliza ugonjwa wa kansa na pili kuna kila dalili hii sumu ya nyuki ule ugonjwa wa ukimwi inaweza kuwa kiboko yake," alisema.
Pinda alisema kutokana na hali hiyo hatupotezi muda katika kumlinda mdudu nyuki ili kuweza kunufaika naye kwani kwa upande wa afya ni chakula kizuri na ni fursa ya uchumi.
"Tumlinde sana mdudu nyuki na wataalam wanatuambia nyuki wakipotea leo ghafla maisha ya mwanadamu yatabaki ni ya mwaka mmoja tu unabaki unaanguka utafikiri umelogwa ,ndo maana tunashauri tumia angalau kijiko kimoja cha asali sababu kuna kila aina ya chakula ndani ya asali," alisema.
Alisema dunia nzima inahangaika na mdudu nyuki kwasababu vyakula vingi duniani ili kupata mbegu au tuna kunatakiwa kufanyike uchavushaji ambao unafanywa na nyuki kwani kwenye mazao yote asilimia 90 yanamtegemea nyuki.
"Ukienda Ulaya nyuki wakipotea kidogo tu yaani hapo itakuwa ni kilio maana bila nyuki hakuna chochote ndo maana dunia nzima inamwangia nyuki kwa jicho kali,"alisema.
Aliongeza kuwa kutokana na mazingira mazuri yaliyopo Tanzania ilistahili kuwa kinara wa uzalishaji wa asali duniani lakini kiwango kinachozaliswa ni tani 35,000 tu.
Pinda alisema Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mkutano mkubwa wa kidunia utaofanyika 2027 ambao utawashirikisha wadau zaidi ya 6000 wa nyuki kutoka nchi 117.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kijiji cha Nyuki Co. Ltd,Philemon Kiemi,alisema katika utafiti alioufanya wa miaka 12 amegundua mazao matano yanayotokana na nyuki tofauti na mwanzo ambapo wafugaji wa nyuki wanafahamu asali na nta tu.
Alitaja mazao ya nyuki mapya kuwa vumbi la Singida ambalo inasaidia nguvu za kiume na inauzwa Sh.laki 3 kwa kilo moja, maziwa ya nyuki yanauzwa Sh.milioni 12 kwa kilo,mkate wa nyuki Sh.300,000,gundi la nyuki Sh.milioni 3 na sumu ya nyuki ambayo inauzwa Sh.milioni 150 kwa kilo.
Kiemi alisema idadi ya makundi ya nyuki yaliyopo katika Mkoa wa Singida inafanana na idadi ya watu waliopo katika mkoa huo lakini makundi yaliyoweza kukaa kwenye mizinga ni 240 tu na yaliyobaki yanakaa kwenye madari,mashimo,ardhini,magome ya miti,zahanati na shule.
"Niwaombe wananchi kuendelea kuweka mizinga ili kuwanusuru nyuki wasikae kwenye zahanati,shule na pia watu wasikate miti badala yake wapande miti ambayo inapendwa na nyuki,"alisema.
"Tunaamini kuwa kama wafugaji wa asili wakipata vifaa vya kisasa kama vile mzinga wa Singida Techno Heifer na kuvuna mazao mapya kama vumbi la Singida pamoja na kupata vifaa vya kujikinga na nyuki wakati wa kulina asali sekta ya nyuki itapaa na kuwainua wananchi wengi nchini kiuchumi," alisema.
Kiemi alisema jukumu kubwa ambalo kampuni ya Kijiji cha Nyuki inaendelea kulifanya ni kuwahakikishia wafugaji wa nyuki Mkoa wa Singida soko la uhakika soko la asali na bidhaa zinazozalishwa kutokana na nyuki katika kiwanda cha kuchakata asali ambacho kipo ndani ya Kijiji cha Nyuki.
Aliongeza kuwa lengo la kampuni ni kutaka kuwawezesha wafugaji wa nyuki waweze kuuza asali na bidhaa zitokanazo na asali kimataifa ambapo ili waweze kufikia hatua hiyo ni lazima wasajiriwe kufanya ufugaji wa nyuki hai (Organic Bee Keeping) ndipo wataweza kuuza asali na bidhaa katika masoko ya nje yakiwa na viwango vya kimataifa na kwa bei kubwa.
Kwaupande wao wafugaji wa nyuki waliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwakopesha fedha zitakazowawezesha kununua mizinga ya kisasa pamoja na kuwatengea maeneo maalumu kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.
Wakati wa mkutano huo wafugaji 500 wa nyuki walipewa mizinga ya nyuki ya kisasa.
0 Comments