Header Ads Widget

SHULE 3000 NCHINI KUSOMA KISHUA KWA MFUMO WA KIDIGITALI


 

 Na John Masanja,Dodoma 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Habari na Mawasiliano imesaini mkataba na wadau UNICEF na Airtel unaohusisha usimikaji wa mfumo mpya wa kidigitali wa Airtel Smart Wasomi kwenye shule 3000, wenye lengo la kuboresha uendeshaji wa shughuli za elimu nchini. 



Tukio hilo limefanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, likishuhudiwa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu kutoka ofisi za serikali pamoja na sekta binafsi.



Akizungumza wakati wa tukio hilo Carolyne Nombo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia alisema mradi huo utaleta faida kubwa katika sekta ya elimu kwa kuboresha upatikanaji wa maudhui ya kielimu kwa njia ya kimtandao na kidigitali.


Aidha, Carolyne alitoa pongezi kwa taasisi ya UNICEF na Airtel kwa ushirikiano na serikali kupitia uanzishwaji wa mradi wa Airtel Smart Wasomi na alisema utakuwa ni nafasi pekee yakuleta mabadiliko chanya katika mfumo wa elimu nchini kupitia matumizi ya tehama.


“kupitia ushirikiano huu ni dhahiri kuwa tunayo nafasi ya kipekee yakuleta mabadiliko chanya katika mfumo wetu wa elimu, kupitia matumizi ya tehama” alisema Carolyne.


Hata hivyo alisema mradi huo unaakisi malengo ya serikali wa kutoa huduma jumuishi kidigitali lakini pia utakwenda kuongeza hari kwa watoto kujifunza hasa kwa shule zenye changamoto ya vifaa vya kutosha vya kujifunzia na kufundishia.


“moja ya jukumu la serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni kuhakikisha tunaendelea kuandaa maudhui ya masomo pamoja na mifumo mbalimbali itakayowezesha ufundishaji na ujifunzaji wa kidigitali katika ngazi zote za elimu” aliongezea Carolyne.


Sambamba na hilo aliendelea kuwakaribisha wadau wengine wasisite kujitokeza na kuendelea kuunga mkono jitihada za kiserikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.



Kwa upande wake Dkt. Emmanuel Shindika kutoka Wizara ya TAMISEMI alisema malengo ya serikali kupitia Rais TAMISEMI ni kuhakikisha shule zina miundombinu stahiki ya utoaji elimu bora na hivyo wanafura na ujio wa teknolojia hiyo na kusema anaamini utaleta mabadiliko katika sekta ya elimu.


“ninaahidi kwamba, tutalinda miundombinu hii ili ifae kwa vizazi vilivyopo, vijavyo mpaka mwisho wa kihama” alihitimisha Dkt. Emmanuel.


Mwl. Beatrice Bongole ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Makole alitoa shukurani zake kwa serikali kwa kuichagua Shule ya Sekondari Makole kuwa ni miongoni mwa shule zinazonufaika na mradi wa Airtel Smart Wasomi na kuahidi kuutunza kwa matumizi sahihi ya kuboresha shughuli za ufundishaji na ujifunzaji.


Naye Maria Jonasi, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Makole alitoa shukuani kwa Serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo na kuahidi wataitumia ipasavyo katika kijupatia maarifa.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI