NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Mwanamke mwenye ulemavu Faustina Urassa ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Songambele Inishiative shirika linalofanya kazi na wanawake, wasichana na watoto wenye ulemavu, amewataka wanawake, wanapoenda kusherekea mafanikio na kuzungumzia changamoto zao kuhakikisha wanawakumbuka na wanawake wenye ulemavu.
Bi Urassa ametoa wito huo wakati akizungumza na Matukio Daima juu ya siku ya wanawake Duniani ambapo alisema ni mara chache sana katika uhamasishaji wanapozungumzia siku ya wanawake kuona wanahamasishwa wanawake wenye ulemavu kushiriki katika siku hiyo hivyo ni vema wakawakumbuka na wao..
“Kundi la wanawake wenye ulemavu tumesahaulika na hii ni kwasababu mtizamo wao wanatuona kama ni wagonjwa, wanatuona kama hatutaweza kutoka ndani, wanatuona kama hatuna mchango wowote katika jamii na pengine wanaona kwamba wanatusumbua lakini sisi tuko sawa,” Alisema.
“Haya ni maisha yetu halisi na kama unavyoona kuna mengi tunafanya kwaajili ya maendeleo yatu na kusaidia jamii na taifa kwa ujumla hivyo ni vema wakati wanapoenda kusherekea mafanikio na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazotukabili kama wanawake wahakikishe na sisi wenye ulemavu tunakumbukwa,” Alisema Faustine Urassa.
Alifafanua kuwa wanapozungumzia siku ya wanawake duniania wanamaanisha wanamke wote bila kujali mtizamo wao, muonekano wao, dini, hali ya kiuchumi na mengineyo ilihali ni mwanamke wote wamejumuishwa kwenye siku hiyo, wanapigania haki zao iwe ni wanamke wenye ulemavu au wasio na ulemavu ambapo wanawake ambao hawana ulemavu moja kwa moja wanapigania haki zao za msingi lakini kukubalika katika makundi mengine mbalimbali na kuzungumzia wanayoyapitia wao kama wanawake.
“Ila linapokuja kwa wanawake wenye ulemavu tunapitia hii mara tatu zaidi, kwanza kama mwanamke na pili kama mwanamke mwenye ulemavu na kwa mantiki hiyo tunatengwa katika jamii lakini kuna wakati pia hata wanawake wenzetu wanatusahau,” Alifafanua
Aliendelea kusema kuwa wanapozungumzia masuala ya usawa wa kijinsia au wanapozungumzia 50/50 kufikia mwaka 2030 bila kuwajumuisha wanawake wenye ulemavu watakuwa hawajafanya kitu kama kweli wanamaanisha 50/50 wahakikishe wanawajumuisha wanawake wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu pamoja.
Hata hivyo siku ya wanawake Duniani inaadhimishwa kila mwaka machi 8 ambapo wanawake wote husherehekea siku hii kwa kueleza nafasi ya mwanamke katika jamii, mafanikio yao na changamoto mbalimbali zinazowakabili kupitia majukwaa na mabango mbalimbali ili kuweza kuzifikisha kwa mamlaka mbalimbali ikiwemo serikali katika kuleta ufumbuzi ikiwemo sera zitakazosaidia kukuza ustawi wa mwanamke.
0 Comments