Na Thobias Mwanakatwe, MKALAMA
WALIMU wanaofundisha darasa la kwanza katika shule za msingi za Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida wametakiwa kutumia vyema mafunzo yanayohusu mtaala mpya ulioboreshwa kwa ajili ya kuondoa tatizo la wanafunzi kutokujua Kusoma,Kuandika na Kuhesabu katika wilaya hiyo.
Kaimu Afisa Elimu ya Msingi Wilaya ya Mkalama, Amina Irumba alitoa wito huo wakati wa mafunzo ya siku tano kuhusu mbinu stahiki za ufundishaji na ujifunzaji wa umahiri wa kiingereza na Kuandika,Kusoma na Kuhesabu kwa kuzingatia mtaaala ulioboreshwa mwaka 2023 yanayofanyika katika ukumbi wa Sheketela uliopo Halmashauri ya wilaya ya Mkalama.
“Tusikilize kwa makini ili tukawe wajumbe wazuri huko tunakokwenda, ni matumaini yangu tunaenda kuondoa KKK katika Halmashauri yetu ya Mkalama. Nachowahidi maafisa kutoka wizara ya Elimu,TAMISEMI hiki kinachofanyika hapa tutakisimamia kwa umahiri mkubwa na kuleta matokeo," alisema Bi. Irumba
Naye Zena Amiri kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) aliwataka walimu hao kuwa wabunifu wa mbinu mbalimbali zitakazowasaidia wakati wa kufundisha.
“Kuweni wabunifu wa mbinu mbalimbali za kufundisha,tumieni mbinu na zana stahiki katika kufundisha stadi za KKK, tumieni TEHEMA katika ufundishaji na ujifunzaji,ubora wa elimu unatokana na ubora wa walimu”, alisema.
Mafunzo haya ya siku tano kuhusu mbinu stahiki za ufundishaji na ujifunzaji wa umahiri wa kiingereza na KKK kwa kuzingatia mtaaala ulioboreshwa mwaka 2023 kwa walimu wa darasa la kwanza yamejumuisha walimu kutoka shule 95 za Wilaya ya Mkalama na yanatarajiwa kuhitimishwa Februari 16, 2024.
0 Comments