NA HADIJA OMARY _LINDI
MKUU wa Mkoa wa Lindi Bi. Zainab Telack amewataka wakazi wa wilaya ya Kilwa na maeneo ya jirani kuchangia fursa za ujio wa Utalii wanaofika katika Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia wa Magofu ya kale Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kutengeneza bidhaa zinazopendwa na watalii na kuwauzia ili kukuza kipato chao
Mhe. Zainab ameyasema hayo Februari 28, 2024 alipokuwa na waandishi wa habari ndani ya Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara wakati wa mapokezi ya Meli ya Kitalii aina ya Le champlain ikiwa na jumla ya Watalii 120 wakitokea mataifa mbalimbali
Watalii hao wamefika katika visiwa hivyo kwa ajili ya kujionea na kujifunza mambo mbalimbali ya Utalii wa kihistoria yaliyohifadhiwa katika kisiwa hicho.
Amesema mfululizo wa safari hizo wa meli za watalii katika kisiwa hicho ni kiashiria tosha kwamba filamu ya Royal Tour iliyochezwa na Rais Samia imeleta matokeo chanya hivyo ni wakati sasa kwa wananchi kuchangamkia fursa zinazotokana na ujio wa watalii hao
Amesema yapo maboresho makubwa ambayo yamefanywa na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo yanawavutia watalii kufika katika hifadhi hizo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ya ki historia na hata kwa wenyeji kuuza bidhaa zinazopendwa na watalii.
Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi hiyo Mercy Mbogelah amesema uwepo wa majengo ya kale yaliyojengwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita kama vile msikiti mkubwa na mkongwe kuliko yote katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki na ngome ya Mreno ni niongoni mwa vivutio vikubwa vya kihistoria vinavyowafanya watalii wengi kumiminika katika Hifadhi hiyo
" kutokana na historia hiyo kubwa ndani ya Hifadhi ya Kilwa kisiwani Mwaka 1981 Shirika la Kimataifa la UNESCO liliipa hadhi Hifadhi hiyo na kuwa Hifadhi ya Urithi wa utamaduni wa Dunia na baadae Mwaka 2023 kuwepa hadhi nyingine kuwa "Man and Biosphere Reserve". Vigezo vyote hivi vimetajwa kuwa mojawapo ya sababu za watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali kupenda kuitembelea hifadhi yetu hii" alisema Mbogelah
Naye Afisa Utalii wa Hifadhi hiyo, Shindawangoni Rajabu amesema toka kufanyike Maboresho ya miundombinu wezeshi ya utalii yaliyofanywa na Serikali kupitia TAWA yamechangia kuwepo kwa ongezeko kubwa la watalii wanaotembelea Hifadhi hizo ambapo mwaka 2024 mpaka kufikia mwezi February wamepokea meli nane tofauti na mwaka 2023 ambapo walipokea meli moja na mwaka 2022 walipokea meli tatu pekee
Kwa upande wake Bibie Ally mkazi wa kilwa kisiwani amesema wao kama wenyeji wa maeneo hayo wanafarijika kuona ujio wa wageni mbalimbali wakifika katika mji huo wa kitalii wa kilwa kisiwani kwani wamekuwa wakiingiza kipato katika kijiji pamoja na mtu mmoja mmoja kutokana na bidhaa wanazoziuza wanapofika watalii.
0 Comments