NA NAMNYAK KIVUYO: TANGA
Ili kulinda misitu wananchi wa Vijiji 20 kutoka halmashauri tano zinazozunguka hifadhi ya mazingira asilia ya Amani (Amani Nature Reserve),wananufaika na ajira ikiwemo za usafishaji wa mipaka,uboreshaji wa barabara za kupita watalii pamoja na miundombinu mingine ya kuvutia utalii.
Aidha wamewezeshwa kwa kupewa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi rafiki ikiwemo ya upandaji miti,utengenezaji majiko sanifu,ufugaji wa Samaki na nyuki ili kupunguza kasi ya uvunaji wa rasilimali za misitu ikiwemo kuni kwa ajili ya kupikia na ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kupasua mbao.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mhifadhi wa hifadhi hiyo ya mazingira ya asilia ya Amani,Nikundiwe Majoya, alisema miradi na ajira hizo kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo imesaidia kupunguza kuingia msituni na kufanya shughuli ambazo siyo rafiki kwatika kuhifadhi mazingira.
Alisema miradi hiyo inatekelezwa na mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF),imesaidia kuongeza mapato ya hifadhi hiyo kutoka milioni 30 kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 hadi kufikia milioni 40 mwaka 2023/2024 na idadi ya watalii katika kipindi hicho ikiongezeka kutoka 3,000 hadi kufikia watalii 4,000.
“Katika hifadhi hii tunahifadhi biaonwai zote ambazo zinapatikana katika msitu huu lakini kupitia ufadhili wa Mfuko huo katika nyanja tofauti ikiwemo doria,ufanyaji usafi katika mipaka njia za watalii,miradi kwa jamii imesaidia kuilinda,”alisema
“Tunaona maboresho ya viumbehai vinazidi kuboreka na hata vilivyokuwa vimetoweka awali sasa vimerejea katika hali yake ya kawaida hasa ndege na viumbe vingine kama vinyonga ambao wanapatikana katika msitu huu,kutokana na kushirikisha jamii kwa kiasi kikubwa kuulinda,”aliongeza
Mmoja wa wanufaika wa ajira hizo,Mrisho Nzota kutoka Kijiji cha Mikwinini,Kata ya Shebomeza,ambaye anahusika na kusafisha mipaka na njia za watalii,alisema kutokana na elimu ya uhifadhi waliyopewa imewasaidia kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira huku ajira hizo zikiwapa kipato kinachowawezesha kuhudumia familia zao.
Alisema awali walikuwa wakiishi maisha magumu kutokana na kutokuwa na shughuli zinazowawezesha kujiingizia kipato ila kwa sasa imewasaidia hadi kuzuia viashiria vinavyoweza kuhatarisha usalama wa hifadhi na kushirikiana kulinda na kudhibiti eneo hilo.
“Baada ya elimu tumegundua kutokulinda mazingira kunachangia wanyama wa asili kutoweka,tunakosa hali ya hewa nzuri,kuharibu vyanzo vya maji,”alisema
Naye Daudi Tofio,mkazi wa Kijiji cha Kisiwani,ambaye ni mkulima na anajishughulisha na kutunza mazingira msituni humo,moja ya mambo wanayofurahia ni pamoja na kupata ajira kutokana na shughuli wanazofanya.
“Sisi kama vijana tunanufaika na kupata ajira,tunashirikiana kama wanajamii kuhakikisha vyanzo vya maji haviharibiwi hivyo tunashukuru sana Mfuko kwa kuangalia suala hili kwani linawezesha tuhudumie familia zetu kikamilifu,”alisema
Ofisa miradi wa Mfuko huo Kanda ya Kaskazini,Magreth Victor,alisema vijiji hivyo vinapatikana katika wilaya tano ambazo ni Muheza,Lushoto,Korogwe na Mkinga (Tanga) na Same mkoani Kilimanjaro.
Alisema kila mwaka wamekuwa wakitoa Sh 49milioni kwa hifadhi hiyo,kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za uhifadhi,utunzaji wa misitu pamoja na utalii ikolojia ikiwemo kusafisha mipaka,kufanya doria na kuboresha vivutio vya watalii ikiwemo malazi.
“Baada ya kuanza kushirikisha wananchi wanaopakana na hifadhi hii, tumeona mabadiliko makubwa kumekuwa na ongezeko la bianonuai,uharibifu umepungua na uelewa wa jamii kuhusu kuhifadhi msitu na vyanzo vya maji umeongezeka,”alisema
“Ukipita kwenye maeneo ambayo mfuko una miradi ya kijamii,unaona namna gani mwananchi anaelewa umuhimu wa misitu na mfano yanapotokea majanga ya moto au uhalifu mwingine ni rahisi mwananchi kutoa taarifa,”alieleza
Muongoza watalii katika hifadhi hiyo,Gabriel Ponera alitaja miongoni mwa vitu vichache vinavyovutia watalii ni pamoja na kinyonga mwenye pembe tatu anapatikana katika milima hiyo pekee na baadhi ya ndege ambao hawaonekani kwa urahisi katika maeneo mengine na kutembea kwa msitu.
“Sisi kama wanavijiji tunanufaika kwanza na elimu ya viumbe hao kama sisi waongoza watalii tunapewa mara kw amara,tunapata kipato na kuhudumia familia zetu,wanavijiji wanapata fursa za kuuza bidhaa kama matunda na viungo,hivyo umekuwa msaada kwetu,”alisema
0 Comments