Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP, Handeni-Tanga.
SERIKALI inatarajia kuwasha mitambo miwili ya kufua umeme toka katika mradi mkubwa wa bwawa la Mwalimu Nyerere katika Mto Rufiji ili kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la kukatika kwa umeme Nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais Mhe.Dkt Philip Isdor Mpango alipozungumza na wananchi wa Kata ya Kabuku Wilayani Handeni Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mkoani hapa.
Dkt Mpango alisema anakubaliana na wananchi wa kata hiyo na Tanzania kwa ujumla ya kuwepo kwa tatizo la umeme ambapo alisema tatizo hilo ni la Kitaifa na sio Mkoa wa Tanga pekee.
Aidha alisema Serikali ilikusudia kuwasha mtambo mmoja mwezi huu wa pili ambapo yapo mambo yaliyosababisha wasitishe zoezi hilo na badala yake mwezi wa tatu mitambo miwili itawashwa ili kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa umeme kwa nchi nzima.
"Tulitarajia mwezi huu kuwasha mtambo mmoja wa umeme tena tulipanga kufanya japo sherehe lakini tumesitisha kutokana na mambo yaliyo nje ya uwezo wetu na sasa tunatarajia mwezi ujao tutawasha mitambo miwili na huu ndio mpango wa Serikali kumaliza tatizo la umeme"Alisema Dkt Moango.
Dkt Mpango aliyasema hayo baada ya wananchi wa kata hiyo ya Kabuku walipomlalamikia kwa kuwepo katizo la umeme jambo ambalo linawakwamisha katika shughuli zao za kila siku za kuwaingizia kipato.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais alimuagiza Mkuu wa Mkoa Tanga na Wakuu wote wa Wilaya Mkoani hapa kuwa wanawasimamia vema wananchi wasiharibu uwoto wa asili na ukataji wa miti hovyo ili kupunguza athari zitokanazo na uharibifu huo.
Makamu wa Rais alisema miongoni mwa majukumu yake ni kusimami mazingira na uwoto wa asili Nchini ili kuhakikisha mabadiliko ya hali ya Nchi yasitokee na kuketa athari kwa wananchi.
"Mkuu wa Mkoa na Madc mpo Tanga uharibifu wa mazingira ni mkubwa sana wasimamieni wananchi wasiharibu mazingira jana Jijini Dar es Salaam joto lilifikia nyuzi 36 hali sio nzuri na hii inatokana na uharibifu wa mazingira"Alisema Dkt Mpango.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba alipokuwa akitoa salamu za Mkoa alisema hali ya usalama kwa upande wa ardhi,majini na ndani na mipaka ya Mkoa ipo salama na hakuna matukio yoyote ya uvunjifu wa amani.
Kindamba alisema mbali na hayo pia hali ya kisiasa iko vizuri huku Serikali ya Mkoa ikiendelea kusimamia vema miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ambapo kwa mika mitatu ya Rais Samia Tanga imepokea zaidi ya Shs tirioni 2.6.
"Mhe,Makamu wa Rais tunayo haja ya kumshukuru Rais wetu kwa kipindi chake cha mika mitatu tumepokea zaidi ya Shs tirioni 2.6 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwetu ni fahari kubwa sana"Alisema Kindamba.
Akiwawakilisha wananchi Mbunge wa Handeni Mji Ruben Kwagwila alisema mbele ya Makamu huyo wa Rais kuwa Kabuku na Handeni kwa ujumla kumekuwepo na katizo la umeme linaloplekea wafanyabiashara wengi kuzorota kwa biashara zao zinazohitaji nishati hiyo.
Kwagwila alisema zipo changamoto nyingi katika kata hiyo ya Kabuku na Wilaya nzima kama vituo vya afya,barabara za ndani lakini zaidi ni tatizo la uhaba wa umeme ambao ndio chachu ya maendeleo katika Wilaya hiyo na Vitongoji vyake.
0 Comments