Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP, Arusha.
SERIKALI inaendelea kutoa kipaumbele kwa wanaosoma masomo ya Sayansi pamoja na kutoa ufadhili wa masomo hayo ili kuongeza hamasa kwa Vijana wa kitanzania wakiwemo wasichana kupenda kusoma masomo hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Mkoani Arusha katika Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi.
Prof Mkenda alisema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika mazingira mazuri kwa ajili ya Vijana kupata fursa mbalimbali katika nyanja za Sayansi za masomo na kuendeleza ubunifu ili kuendana na kasi ya teknolojia duniani na hata soko la ajira ndani na nje ya nchi.
"Taifa lina upungufu wa Wanasayansi na hasa Wanawake na Wasichana, kwa sababu ni wachache wanaosoma ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) hivyo tutaendelea kuhamasisha wasichana kupenda na kujiunga na masomo hayo". Alisema Mkenda.
Aidha alisema kuwa ili Taifa liendelee linahitaji Wanasayasi hivyo Serikali kupitia Wizara na Wadau mbalimbali wataendelea kufungua fursa na kuweka mazingira sahihi ya ujifunzaji katika Sayansi.
Alibanisha kuwa Serikali inatekeleza baadhi ya afua ili kuongeza idadi ya wataalam wa Sayansi
Wanawake ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili wa masomo ikiwemo Samia Scholarship na Mikopo ya kujenga Shule za Sekondari Maalum za Sayansi za Wasichana kila Mkoa.
Prof Mkenda alisema mbali na hayo pia Serikali inazidi kuimarisha mafunzo ya Ualimu wa Sayansi, kufanya mapitio ya sera ya sayansi Teknolojia na Ubunifu na kupitia mitaala mipya kutoa msukumo katika masuala ya kuwezesha wanafunzi kuwa na fikra tunduizi na kutoa kipaumbele katika somo la TEHAMA ambapo wataandaa wanasayansi wa kuwezesha kwenda sambamba na mapinduzi ya nne ya viwanda.
Mkurugenzi wa Elimu Endelezi kutoka Taasisi ya STEM katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) Dkt. Leonard Mwalongo ameishukuru Serikali Kwa kutoa ufadhili wa masomo ya Sayansi kwa Wasichana waliopungukiwa sifa za moja kwa moja za kujiunga na Vyuo Vikuu katika kozi za Sayansikupitia foundation program ya Mwaka mmoja inayotolewa na OUT.
"Ufadhili huu ni asilimia mia moja unatolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa miaka 5, tunatarajia kufadhili Wanafunzi 1,000 ambapo kila mwaka 200 watanufaika". Alisema Dkt. Mwolongo.
Akiwasilisha mada Mzungumzaji Mkuu Prof. Verdiana Masanja alisema kwa Tanzania ni asilimia 12 pekee ya Wanawake ndio wapo katika Uongozi wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM).
Prof Verdiana aliswma huu ni wakati muafaka kuwahimiza Wasichana na Wanawake pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya kusaidia ukuaji wao katika masuala ya uongozi, taaluma na ujasiriamali.
"Ila mbali na yote lakini tunapaswa tusisahau kuliandaa kundi hili kuingia katika mapinduzi ya nne ya Viwanda yakisukumwa na teknolojia mpya ikiwemo _AI (Artificial Intelligence ) na IOT (Internent of Things)"Alisema Prof Verdiana.
0 Comments