Na Fadhili Abdallah,Kigoma
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Kigoma imeanza msako kumtafuta Mwalim Mkuu wa shule ya Msingi Businde manispaa ya Kigoma kwa tuhuma za kukimbia fedha za utengenezaji wa madawati ya shule hiyo kiasi cha shilingi milioni 15.
Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoa Kigoma, John Mgallah akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa niaba ya Kamanda wa TAKUKURU mkoa Kigoma, Stephen Mafipa kuhusiana na ufuatiliaji wa miradi 25 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi Bilioni 9.4 yenye mapungufu.
Mgallah alisema kuwa shule hiyo iliingiziwa fedha za utekelezaji miradi ya madarasa ikiwemo fedha za utengenezaji wa madawati ndipo mwalim huyo Mkuu alitaka kukata miti inayozungusha shule hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa jambo hilo ambapo wazazi walikataa mpango huo.
Baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa jambo alisema kuwa TAKUKURU walianzisha uchunguzi na kuthibitisha uwepo wa jambo hilo hivyo kupata kibali cha kumfikisha mtuhumiwa mahakamani ambapo hata hivyo Mtuhumiwa alikimbia na sasa anatafutwa.
Katika tukio lingine Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoa Kigoma inafuatilia matumizi yenye mashaka ya ujenzi wa shule ya sekondari Businde na nyumba za walimu ambapo uchunguzi wa awali unaashiria kuwepo kwa vitendo vya ubadhirifu kwenye mradi huo.
Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoa Kigoma, John Mgallah alisema kuwa tayari timu ya uchunguzi imeshaanza kuufanyia ufuatiliaji na itatoa taarifa kuhusiana na hatua zitakazochukuliwa baada ya uchunguzi huo.
0 Comments