Header Ads Widget

CHUO CHA ST. MAGDALENA CHAPOKEA VIFAA TIBA KUKABILIANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

 


Na Mwandishi wetu, Kagera

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha St. Magdalena–Mugana, Dr. Dunstan Bishanga, amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa hatari kubwa kwa sasa, na kusisitiza umuhimu wa jamii kujikinga na magonjwa hayo mapema badala ya kuwekeza zaidi katika matibabu baada ya kuugua.


Akizungumza Desemba 31, 2025, wakati akiongoza viongozi wa Hospitali ya Mugana pamoja na wanafunzi wa Chuo hicho kupokea vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili vilivyotolewa na kundi la wanamichezo la Bwanjai Veterans kutoka Kata ya Bwanjai, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, Dr. Bishanga alisema kuwa kwa sasa magonjwa yasiyoambukiza ni tishio duniani, hivyo vifaa hivyo vitasaidia jamii kutambua hali zao za kiafya mapema.


“Tumeona wadau wa Bwanjai Veterans wametupatia vifaa vya kufanya vipimo vya baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo kisukari. Hili ni jambo la kupongeza kwani linaongeza nguvu katika kufikisha huduma kwa jamii zetu, hasa ikizingatiwa kuwa magonjwa haya yamekuwa tishio kubwa. Hata hivyo, nasisitiza kuwa ni muhimu zaidi kuwekeza katika elimu kwa jamii ili kuchukua tahadhari mapema badala ya kupambana na magonjwa yanapojitokeza,” alisema Dr. Bishanga.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bwanjai Veterans, CP Justus Kamgisha, alisema kuwa vifaa hivyo vimetokana na michango ya wadau ambao ni wachezaji wa zamani kutoka Kata ya Bwanjai, waliounda kikundi hicho kwa lengo la kuwaleta pamoja, lakini baadaye kupanua wigo wa huduma zao kwa jamii.


“Tulianzisha kikundi hiki tukiwa na lengo la kuwaunganisha wachezaji wa zamani wa Bwanjai, lakini kwa sasa tumepanua malengo yetu ili kugusa zaidi jamii zetu. Leo tumefanya hili Mugana, na siku nyingine tunaweza kurudi hapa au kwenda sehemu nyingine, lengo letu ni kuigusa jamii yetu,” alisema Kamgisha.


Aidha, mwanafunzi wa Chuo cha St. Magdalena, Aleta Amon, akisoma taarifa fupi kuhusu huduma zilizotolewa na Chuo hicho kwa kushirikiana na Hospitali ya Mugana, alisema kuwa zoezi la kupima magonjwa yasiyoambukiza lilifanyika katika vijiji vitatu vya Kata ya Bwanjai kuanzia Desemba 11 hadi 18, 2025, vikihusisha vijiji vya Rwamashonga, Buhekera na Buhanga.


Alisema zoezi hilo lililenga kubaini wanakijiji wenye changamoto za magonjwa yasiyoambukiza ambao hawajaanza matibabu, pamoja na wale ambao tayari wameanza.


Aliongeza kuwa zoezi hilo lilihusisha vipimo vya shinikizo la damu (presha), kisukari, pamoja na utoaji wa elimu ya afya hususan kwa wajawazito. Jumla ya wananchi 59 walihudumiwa, wakiwemo watu wazima 51 na watoto wanane. Kati ya watu wazima 51 waliopima presha, wanne waligundulika kuwa na shinikizo la damu, huku kati ya watu 52 waliopima kisukari, wanane walibainika kuwa na kiwango cha juu cha sukari mwilini.


Hata hivyo, katika utekelezaji wa zoezi hilo, walibaini changamoto mbalimbali zinazoweza kuwa kikwazo katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo. Changamoto hizo ni pamoja na ucheleweshwaji wa taarifa kutoka kwa viongozi kwenda kwa wananchi, hali inayosababisha idadi ndogo ya wananchi kujitokeza kupokea huduma.


Changamoto nyingine ni uhaba wa vifaa tiba, ikiwemo mashine za kupimia kisukari, baadhi ya wananchi kushindwa kupata huduma kutokana na changamoto za kiuchumi, ukosefu wa usafiri maalum kwa wataalamu wa afya kufika vijijini, pamoja na ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wahudumu wa afya ngazi ya kijiji kutokana na madai ya kukosa posho. Aidha, baadhi ya wananchi walionyesha uelewa mdogo kuhusu uzingatiaji wa vipaumbele kwa makundi maalum wakati wa utoaji wa huduma.


Baada ya kubaini changamoto hizo, wadau hao walijitolea kiasi cha takribani shilingi milioni moja ili kuwezesha hatua za awali za kuwapeleka wataalamu wa afya katika jamii, ikiwemo kugharamia usafiri na posho. Wito umetolewa kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza kuunga mkono juhudi hizo.


Sambamba na hayo, akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa Chuo cha St. Magdalena, Sr. Editha Karia, aliwashukuru wadau wa Bwanjai Veterans kwa kujitolea kwao, akisema kuwa vifaa hivyo vitakuwa msaada mkubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa jamii.


Ikumbukwe kuwa Hospitali ya Mugana ipo mkoani Kagera na inasifika kwa usafi wa mazingira, ambapo miaka mitatu iliyopita ilitwaa tuzo ya usafi wa mazingira kwa hospitali za wilaya.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI