Katibu wa siasa, uenezi na mafunzo CCM Taifa Paul Makonda akipokewa wilayani Kakonko mkoani Kigoma akiwa kwenye pikipiki ya matairi matatu maarufu kama Guta alipowasili mkoani Kigoma ambapo anafanya ziara ya kichama ya siku mbili mkoani humo
xxxxxxxxx
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Katibu wa idara ya siasa, uenezi na mafunzo Paul Makonda ametoa kiasi cha shilingi milioni tano kwa Mama Imaculata Liston Kisanga mkazi wa wilaya ya mkoani Kigoma kuanzisha mradi utakaomuingizia kipato baada ya kulalamika kuachwa na mume wake kwa kile anachoeleza kushindwa kupata mtoto kwa miaka 15 ya ndoa yao.
Makonda alichukua uamuzi huo baada ya kusikiliza maelezo ya pande mbili ikimuhusisha mwanamke huyo na mume wake ambaye ni Meneji wa TANESCO wilaya ya Kakonko katika maelezo yalioonyesha kwamba mgogoro huo wa ndoa unaonekana kutopata muafaka wa wawili hao kuendelea kuishi pamoja kwa siku za karibuni.
Katibu huyo Mwenezi wa CCM alisema kuwa katika hali inayoonyesha kuhusiana na maelezo yaliyotolewa ni wazi hakuwezi kuwa na muafaka kwa wanandoa hao kwa siku za karibuni hivyo amekabidhi fedha hizo kwa mwanamke huyo ili ziweze kumsaidia katika Maisha yake mapya.
Kabla kufikia uamuzi huo Makonda alimwita Meneja huyo wa TANESCO na kumuomba walimalize suala hilo na warudiane waishi Pamoja kwani haina afya kuwa na migogoro ya ndoa isiyoisha majibu ya mwanaume huyo inaonyesha hakuwezi kuwa na maelewano kwa sasa.
Awali mwanamke huyo akitoa maelezo kwa Katibu Mwenezi wa CCM Taifa alisema kuwa amefukuzwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na mume wake sababu kubwa ikiwa ni kutopata mtoto na sasa hana mahali pa kuishi baada ya mahakama kumpa haki mume wake ya kuendelea kumiliki nyumba hizo.
Akizungumza mbele ya Katibu Mwenezi wa CCM Taifa Meneja huyo wa TANESCO wilaya ya Kakonko, Enock Bwire katika maelezo yake alisema kuwa mgogoro wao wa ndoa umechukua miaka 10 sasa na kufikia kulifikisha suala hilo mahakamani ambapo mahakama imetoa hukumu ya wanandoa hao kutengana kwa muda.
Alisema kuwa licha ya hukumu hiyo bado mwanamke huyo anaishi nyumbani kwake hadi wakati huo (jana) ambao walikuwa wamesimama mbele ya Katibu huyo Mwenezi wa CCM kutokana na mwanamke huyo kutokubaliana na uamuzi wa kutengena na Kwenda kwao.
Bwire alisema kuwa hana tatizo na mke wake lakini kwa sasa anaheshimu hukumu ya mahakama ambayo imetoa uamuzi wa wawili hao kutengana na kwamba kama kuna mgawanyo wa mali vyombo vya sheria vitatoa maamuzi.
0 Comments