Na;Kiobya shamteabas@gmail.com)
Mafuriko ya wananchi kwenye mikutano ya Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Paul Christian Makonda, yanafikirisha na kutoa taswira ya misukosuko ya kilichowahi kutokea nchi za ulaya na Himaya Takatifu ya Kirumi (Roman Empire) karne kadha zilizopita. Je, taswira hii inatokana na nini? Je, msukumo wa mafuriko hayo, hasa, ni kitu gani? Ni mapenzi na imani ya wananchi kwa Rais, Ni mapenzi na imani kwa Chama Cha Mapinduzi? Ni mapenzi na imani kwa Serikali ya awamu ya sita? Ni mapenzi na imani kwa Katibu Mwenezi wa CCM? Au ni mafuriko ya wananchi ambao wanakufa maji, wanatapatapa, wamekata tamaa, hawana matumaini?
Kuteuliwa kwa Paul Makonda kuwa Katibu Mwenezi wa CCM kumeamsha vuguvugu la aina yake miongoni mwa wananchi. Tangu aanze ziara za kikazi nchini, wananchi wamekuwa wakikusanyika kwa wingi, pengine mikusanyiko hiyo ifananishwe na mafuriko! Iwe kwenye barabara anakopita au kwenye mikutano anayofanya. Kwa hiari yao, wananchi wanakusanyika bila kusombwa na magari au hata kuwekewa vivutio vya wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya.
Kila anakopita, kila anakokwenda, ujio wake unasubiriwa kwa matumaini makubwa, kama vile mwokozi.
Wananchi wanatoa yaliyo katika mitima yao; wanalalamika kwake, wanamweleza wanavyonyanyaswa, wanavyodhulumiwa, wanavyopuuzwa. Katika mazingira kama haya, Katibu Mwenezi wa CCM anajikuta akitekeleza majukumu ya mahakama, polisi, TAKUKURU, diwani, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, na hata waziri! Majuzi, akiwa mkoani Mwanza, hata alitawazwa kimila kuwa msaidizi wa Hangaya! Pengine hapa turejee tena kile kilichodaiwa kuwa Himaya Takatifu ya Kirumi. Inaeleweka?
Ni vyema kujaribu kutengua kitendawili cha kufurika kwa wananchi wakati wa ujio wa Katibu Mwenezi wa CCM; kukitazama kwa mapana na marefu yake, pia kukichukulia kama shamba darasa! Mafuriko hayo yawe somo kwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali. Walakini, wananchi wanaofurika hawasifii (kama ambavyo ingetarajiwa!) yale ambayo yamefanywa, au kuendelea kufanywa, na serikali ya awamu ya tano: ujenzi wa mahospitali, shule, masoko, stendi za magari, na miundombinu muhimu kwa jumla.
Hata na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutoa hadhari kwamba "serikali kujenga majengo na vitu si hoja wala kipaumbele kwa wananchi, bali jambo muhimu ni kumaliza shida zao ndogo na kubwa zinazowazunguka. Serikali ikishindwa kutekeleza au kupuuza hayo, siku zake zinahesabika; kuna siku italia kilio kwa kuadhibiwa kwenye sanduku la kura".
Ieleweke kwamba ustawi wa wananchi si uwepo wa majengo na miundombinu tu; bali pia usimamizi wa ufanisi wa mifumo ya kiutendaji, serikalini kwenyewe na kwenye taasisi zake.
Kulinda na kutetea uhuru wa raia, haki yao ya kuishi, haki ya kumiliki mali bila kubugudhiwa/kudhulumiwa, na kupambana na rushwa bila ajizi.
Mbali na vioja vya Katibu Mwenezi wa CCM, kipaji chake cha kujieleza pamoja na ubunifu wake wa kusikiliza kero za wananchi ambazo zimekithiri, imedhihirika kwamba kumbe watendaji serikalini hawawajibiki ipasavyo.
Majuzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa kebehi kwamba wananchi wanajisomba kwenye mikutano ya Katibu Mwenezi wa CCM; na wengine wanakimbilia makanisani kumlilia Mungu ili amalize shida zao. Alidai kuwa wanafanya hivyo kutokana na kutojua ni wapi wapeleke shida zao ili zitatuliwe.
Siamini kama wananchi hao ni mbumbumbu kiasi hicho! Ukweli ni kwamba hatua hizo wanazochukua zinadhihirisha kukata tamaa na kutokuwa na imani na taasisi zinazopaswa kusimamia na kutetea haki.
Kero ambazo zimekithiri zinazotajwa kwa Makonda kila anapokwenda ni: rushwa, ufisadi, dhuluma, uonevu, husuda na upendeleo. Wananchi wana imani na Paul Makonda kwa vile "anadiriki" kushughulikia kero zao papo kwa papo, zege halilali.
Hivyo basi, suala la kwa nini wananchi wanafurika kwenye mikutano ya Katibu Mwenezi wa CCM litapata ufumbuzi iwapo mifumo ya utendaji na muundo wa serikali utafumuliwa na kusukwa upya. Kubwa zaidi ni kuwa na katiba mpya ambayo itazingatia mapungufu ambayo yamesheheni kwenye katiba inayotumika hivi sasa.
0 Comments