Header Ads Widget

CCM YAJIVUNIA MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO, YAHAIDI KUBORESHA ELIMU, MAJI NA VIPAJI VYA VIJANA

 

Na Hamida Ramadhan MatukioDaima Media, Dodoma

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema mafanikio ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ni kielelezo cha dhamira yake ya kweli katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, na kwamba kinaendelea kujipanga kuimarisha huduma muhimu za kijamii katika kila sekta.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika Jiji la Dodoma, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, amesema pamoja na mafanikio ya miradi kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA, na barabara kuu za lami, CCM ina mpango kabambe wa kuwekeza zaidi katika elimu, maji, miundombinu ya afya na kukuza vipaji vya vijana.


“Huduma bora kwa wananchi ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli. Tutaendelea kupeleka umeme kwenye vijiji vilivyobaki, kuboresha miundombinu ya shule na zahanati, na kuhakikisha kila kijiji kinapata maji safi na salama,” amesema Mavunde.

Ameeleza kuwa serikali kupitia CCM inaendelea kutekeleza programu maalum za kuibua na kukuza vipaji vya vijana kupitia sekta za michezo, sanaa na ujasiriamali, kwa lengo la kuwapa vijana nafasi ya kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela, amewahimiza wanachama wa chama hicho kutobweteka na mafanikio yaliyopatikana, bali kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ili kuhakikisha CCM inaendelea kuongoza kwa kishindo.

“Ushindi hauji kwa maneno tu, unapatikana kwa vitendo ni wajibu wetu kujitokeza kwa wingi kupiga kura, ili tuendelee na kasi hii ya maendeleo,” amesema Mongela.
Aidha ,aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Benedicto Komba, alitangaza kujiunga na CCM, akieleza kuwa amefanya hivyo kutokana na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya uongozi wa chama hicho


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI