Header Ads Widget

KAMATI YA BUNGE YATOA MAAGIZO HAYA KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA MANYONI

 



Thobias Mwanakatwe,  MANYONI 


KAMATI ya Kudumu ya Bunge,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida kuweka mkakati wa kurejesha haraka Sh.bilioni 1.5 walizokopeshwa na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya Mradi wa Kupanga,Kupima na Kumilikisha Mashamba ya Korosho.


Aidha, kamati hiyo imeiagiza halmashuri hiyo kutoa taarifa inayojitosheleza ambayo itaeleza kwa kina kuhusu mradi huo ili kujua changamoto na kama kuna matatizo ieleze ni nani alisababisha hilo na hatua gani zimechukuliwa.


Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Justin Kamonga, akitoa maazimio ya kamati jana (Februari 10, 2024) baada ya wabunge kutembelea mashamba ya mradi huo na kutoridhishwa na hali ilivyo,alisema taarifa iliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni haijajitosheleza.


"Kufiatia maelezo yaliyopi kwenye taarifa mliyotusomea kamati inashindwa kushauri kuhusu mradi huu kwa hiyo tunaitaka halmashauri iwasilishe taarifa nyingine kwa kamati kabla ya vikao vya bajeti havijaanza mwezi Machi 2024,pia fedha hizi ni mkopo tunahitaji mkakati wa halmashauri wa jinsi ya kuzirejesha" alisema Kamonga.



Naye Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tabora, Hawa Mwaifunga,alisema kwa jinsi hali ilivyo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni haiko 'serious' katika mradi huo na ndio maana katika Sh.bilioni 1.5 walizokopeshwa tangu 2021 wamerejesha Sh.milioni 365.9 tu.


"Mkurugenzi hizi fedha tunazihitaji kama tulivyokubaliana,fedha hizi ni za wananchi zinahitajika na sehemu nyingine msifikiri ni Manyoni tu ambao mnazihitaji,haiwezekani tangu 2021 ni karibu miaka minne sasa hamuonyeshi Dalglish kuzirejesha angalie tusije tukakosesha bajeti yenu,"alisema Mwaifunga.


 Mbunge wa Buchosha  Erick Shigongo alisema iundwe timu maalum kufuatilia madeni ya Sh.milioni 332 ambazo wanadaiwa wananchi waliouziwa mashamba mapya lakini hawajalipia na pia halmashauri itangaze mradi huu ili watu wengi wajitokeze kununua mashamba.



Mbunge wa Temeke,Dorothy Kilave, alisema inatia mashaka kama fedha zilizokopeshwa kwa halmashauri hiyo zitarejeshwa kwasababu kati ya ekari 969.44 zilizorejeshwa kwa wakulima waliokuwa wanaidai halmashuri ekari 479 zimefanywa kuwa barabara.


Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tanga,Mwantumu Zodo,alisema inashangaza kuona kasi ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni katika urejeshaji wa fedha walizokopesha ni ndogo wakati zipo halmashauri nyingine ambazo zilikopesha pamoja na Manyoni zilishamaliza kulipa mkopo huo.


"Suala la kusafisha mashamba ni kazi yao sisi tunachotaka ni pesa hii kasumba ya halmashauri kurejesha kidogokidogo mkopo sio sawa,halmashauri ipo hali mbaya katika kurejesha fedha hizo za mkopo,"alisema.



Mbunge wa Mbulu Mjini,Zacharia Issaay,alisema taarifa ya halmashauri haijitoshelezi kwani haijaeleza kampuni iliyopewa zabuni ya kusafisha mashamba hayo ilianza lini kazi hiyo na ilitakiwa kumaliza lini.


Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba alisema kimsingi mradi huu makosa yalifanyika tangu mwanzo kwani awali gharama za kusafisha shamba ziliwekwa kuwa ni Sh.20,000 hadi 60,000 lakini baadaye ikaja kubainika kiasi hicho ni kidogo kikaongezwa hadi kufikia Sh.273,000 kwa kila shamba.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,Jimson Mhagama alisema hadi kufikia Februari 7, 2024 ekari 1,396 zenye thamani ya Sh.milioni 698 zimeuzwa ambapo fedha zilizokusanywa ni Sh milioni 365.9 bado Sh.miioni 332 hazijalipwa.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI