Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP, Handeni
CHAMA cha Mapinduzi Mkoani Tanga kimepokea wanachama 26 toka cuf wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa viti maalum kupitia Chama hicho Sonia Magogo.
Jana Februari 10 aliyekuwa Mbunge wa viti maalum kupitia Chama hicho Sonia Magogo na wenzake wamefanya maamuzi magumu ya kutimkia CCM kwa kile wanachodai kumuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Dr Samia Suluhu Hassan.
Wanachama hao wa CUF walitangaza nia yao ya kuhamia CCM katika mkutano wa hadhara wa Chama hicho uliofanyika katika uwanja wa sokoni Chanika Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Magogo alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi katika Mkutano huo na alisema kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia na wasaidizi wake ndani ya Chama na Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi na kujenga usawa ni miongoni mwa vitu vilivyowasukuma kuungana nae.
Magogo alisema si muda wa kuvutana kisiasa na kuongeza kuwa wakati umefika wa kuunganisha nguvu na kukisaidia chama cha Mapinduzi na Serikali yake kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma za kijamii na kutatuliwa kero zinazowakabili katika maeneo yao.
"Tunaona kazi ya Mama Samia sio ndogo maendeleo yanakuja kwa kasi na sio yeye tu hata wasaidizi wake hasa ndani ya chama wanafanya kazi kubwa na kwa kweli wanahitaji kuungwa mkono kwa maslahi ya kuwasaidia wananchi na Taifa kwa ujumla"Alisema Magogo.
Magogo ambae pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Jumuiya ya wanawake CUF Taifa alitumia jukwaa hilo kuwaomba wanaccm wawapoke na kuwapa ushirikiano ili azma yao ya kukipigania chama hicho na kuwasaidia wananchi iweze kutimia
Akimpokea wanachama hao wapya,Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Tanga Rajab Abdulrahman alikiasa chama chake kuondoa hofu kwa wanachana wanaohamia wakitokea upinzani na badala yake kitoe ushirikiano kwa wanachama hao wapya na ikibidi watumike katika mikutano ya hadhara.
Rajabu alisema Chama cha Mapinduzi kina misingi imara iliyojengwa na waasisi wa chama hicho hivyo hakuna sababu ya kujenga hofu kwa wanachama wapya wanaotoka upinzani jambo bora ni mshikamano utakaokuwa na tija ndani ya chama kwa maelengo yaleyale ya kuwatumikia wananchi.
"Tuache nongwa najua hofu za wanaccm wenzangu,jamani hawa ni ndugu zetu wamerudi nyumbani na labda nikuombe Mwenyekiti wa CCM Wilaya fanyeni mikutano ya hadahara na muwatumie hawa wananchama wapya msiwaache wakapotea au siku moja wakarudi walipotoka"Alisema Rajabu.
0 Comments