Na Thobias Mwanakatwe, MANYONI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida imekusanya kiasi cha Sh.bilioni 18 sawa na asilimia 62 ya makadirio ya Sh.bilioni 29 hadi kufikia Januari 2024 katika vyanzo mbalimbali vya mpato kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,Jumanne Mlagaza,akizungumza juzi wakati akifungua kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo,alisema kati ya fedha hizo Sh.bilioni 1.8 zimekusanywa kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani.
Alisema katika katika kipindi hicho halmashauri hiyo imepokea Sh.bilioni 5.8 kutoka serikali kuu na wafadhili ambazo zimetumika kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika ngazi ya kata na vijiji.
Mlagaza aliwataka wataalam na viongozi kila mmoja atimize wajibu wake kikamilifu kwa kushirikiana na madiwani katika kusimamia miradi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato pamoja na usimamizi wa fedha kwa ustawi wa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na taifa kwa ujumla.
"Madiwani na watendaji tuna jukumu la kusimamia fedha zinazoletwa na serikali kwenye halmashauri yetu ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudia,nisisitize upendo miongoni mwa madiwani na watendaji na tujenge utamaduni wa kushuka chini kusikiliza kero za wananchi," alisema Mlagaza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,Jimson Mhagama, alisema kila mtendaji atimize wajibu wake katika eneo lake na kwamba ikitokea kuna tatizo atawajibike yeye kama yeye na si vinginevyo.
Kuhusu fedha zaidi ya Sh.bilioni 1.4 zilizoletwa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali ya Wilaya,alisema haziwezi kubadilishwa matumizi na kwamba wanaotaka fedha hizo zipelekwe kwenda kuanzisha ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya hilo kamwe haliwezi kutekelezwa.
"Kama tunataka kujenga hospitali mpya ya wilaya, hivi karibuni tutaanza vikao vya bajeti tuweke suala hili kwenye bajeti ijayo kwamba tunaomba Sh.bilioni 2 au 3 kuanza ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya lakini sio hizi fedha zilizoletwa ndo tuzichukue kwenda kuanzisha ujenzi hilo halitekelezeki," alisema.
Mhagama alisema yapo maneno kwamba baadhi ya majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni ambayo yamechakaa halmashauri inataka kuyabomoa jambo ambalo si la kweli.
Hatua ya Mkurugenzi huyo kutoa ufafanuzi huo ilitokana na madai ya baadhi ya madiwani kutaka fedha zilizoletwa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Hospitali ya Wilaya zibadilishwe matumizi.
Katika hatua nyingine, mradi wa kuchimba visima 11 unaogharimu zaidi ya Sh.milioni 363.3 katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida umekwama kuendelea baada ya mkandarasi aliyepewa zabuni hiyo kutoonekana eneo la kazi huku akiwa ameshalipwa Sh.milioni 73.
Kaimu Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Bernard Marcely alieleza hayo wakati akijibu maswali ya madiwani ambao walihoji kutokamilika kwa miradi ya kuchimba visima kwenye kata zao.
Marcely alisema kampuni ya Coyesa Co.Ltd ilipewa zabuni ya kuchimba visima 11 Wilayani Manyoni kwa gharama ya Sh.milioni 363.3 kazi ambayo kampuni hiyo ilitakiwa kuikamilisha katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ambao umeisha Juni mwaka jana kulingana na mkataba.
Alisema mkandarasi huyo tangu apewe kazi hiyo na kulipwa Sh.milioni 73 amechimba visima vitano tu ambavyo vinatoa maji katika vijiji vya Mbwasa,Majiri,Igwamalete na Makasuku ambapo baada ya hapo ameingia mitini na hajulikani alipo.
"Mkandarasi huyu kila tukimpigia simu aje kwenye kikao haji na hajaonekana 'site' tangu November 2023 na kimsingi Sh.milioni 73 alizolipwa ambazo zinatolewa na Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ambao upo chini ya Wizara ya Maji hazilingani na kazi aliyokwisha ifanya," alisema.
Marcely alisema kutokana na ukaidi wa mkandarasi huyo RUWASA imeanza mchakato wa kuvunja mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine ambaye atafanya kazi ya kuchimba visima sita vilivyobaki.
Madiwani kwa upande wao waliitaka RUWASA kuvielekeza Vyombo vya Utoaji wa huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) ziwe zinatoa taarifa ya mapato na matumizi ya maji kwa jamii.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni,Jumanne Mlagaza,alisema kama CBWSOs hazitajenga utamaduni wa kutoa taarifa ya mapato na matumizi miradi ya maji inaweza kufa pengine kutokana na usimamizi na matumizi mabaya ya fedha za maji.
Hata hivyo, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni, Marcely alisema baadhi ya CBWSOs hazifuati maeelekezo lakini ofisi ya RUWASA inaendelea kuwaelekeza na kuwajengea uwezo viongozi wa vyombo hivyo kufuata sheria na miongozo iliyotolewa na RUWASA.
MWISHO
0 Comments