Header Ads Widget

DARAJA LA MINYUGHE LILILOBOMOKA MWAKA JANA KUIGHARIMU SERIKALI BIL.2/-

 

Na Thobias Mwanakatwe,IKUNGI

WANANCHI zaidi 20,000 wa kata za Minyughe na Makilawa wilayani Ikungi mkoani Singida ambao kwa  miezi minne sasa wamekosa mawasiliano kutokana na kukatika kwa daraja la Minyughe wameanza kupata matumaini baada ya serikali kuanza kulijenga ujenzi utakaogharimu takribani Sh.bilioni 2 hadi kukamilika.


Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahimu Kibasa, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kuwa daraja hilo ambalo lilikatika tangu Oktoba mwaka jana limeanza kujengwa na utekelezaji wake umefikia asilimia 60 na linatakiwa kukamilika Mei 18, 2024. 



Alisema hadi sasa kazi zilizofanyika ni kutengeneza njia ya mchepuko,kupanga mawe na kusuka nondo,kumwaga zege la chini na la juu na ulindaji wa daraja kwa kutumia mawe ambapo mkandarasi wa kampuni ya JP Traders Limited aliyepewa kazi hiyo kwa kulijenga kwa Sh,milioni 556.140, ameshalipwa Sh.milioni 224.770 sawa na asilimia 40.4 ya thamani ya mkataba wote.


Kibasa alitoa mchanganuo kuwa gharama za kununua vyuma vitakavyowekwa juu ya daraja hilo vinagharimu Sh.milioni 939 hivyo jumla ya mradi ni Sh.bilioni 1.4 ambao zikijumlishwa gharama za kodi bandarini na usafirishaji kutoka Dar es Salaam kuja Singida gharama zote za mradi zitafikia takribani Sh.bilioni 2 kasoro.


Kibasa alisema daraja hilo litakapokamilika kujengwa kitakachofuata ni kujenga barabara ya Mtamaa-Minyughe hadi Mtavira kwa kiwango cha changarawe ambapo katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 unaoanza Julai mwaka huu zimetengwa Sh.milioni 360.


“Barabara ya Mtamaa-Minyughe hadi Mtavira ambayo daraja hili lipo ni ya muhimu sana kwa wananchi wa kata za Minyughe na Makilawa kwani maji yakijaa katika daraja wanafunzi wanashindwa kwenda shule au wananchi kushindwa kufuata huduma za matibabu.”alisema.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Serukamba baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo aliagiza juhudi ziongezwe ili liweze kukamilika haraka na wananchi waanze kusafiri kutoka upande wa kata ya Minyughe kwenda upande wa Makilawa. 



Alisema pia daraja hilo litakapokamilika TARURA ihakikishe barabara ya inachongwa vizuri ili iweze kupitika muda wote na katika bajeti ijayo ifikirie namna ya kulinda Mto Saiwa ili usiweze kuathiri daraja baadaye hasa kutokana mwenendo wa mto huo kupanuka kila mara.


“Mto huu unasogea kila wakati na kupanuka hivyo tusipofanya jitihada za kuulinda itafika wakati daraja litaelea pekee yake na kuhatarisha likabomoka wakati limejengwa kwa gharama kubwa,”alisema.


“Utaona gharama za ujenzi wa daraja hili ni takribani Sh.bilioni 2 ambalo linahudumia kata tatu tu pesa kama hizi tulizoea kuona zinatumika kujenga daraja ya kuunganisha wilaya kwa wilaya au mkoa kwa mkoa lakini rais wetu Samia Suluhu Hassan ameona angala kijiji kwa kijiji kiweze kupitika, wananchi tumshukru sana rais,” alisema.


Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi kuongeza juhudi katika kilimo kwani daraja na barabara itakuwepo kwa ajili ya kuwarahisishia kusafirisha mazao yao kwa ajili ya kuyapeleka kwenye masoko.


Alisema wananchi wabadailike katika kilimo kwa kuhakikisha wanaongeza matumizi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji wa mazao.


“Wanasayansi wanasema ekari moja ya mahindi ukiweka mifuko mitano miwili ya kupandia,mitatu ya kukuzia unapata unapata maguni 30 hadi 35 kwa ekari moja lakini leo nyie mkipata zaidi ni maguni mawili au matatu,lazima tutoke huko namna ya kutoka ni kuongeza matumizi ya mbolea,”alisema Serukamba.


Naye Diwani wa Kata ya Minyughe, Nelson Kiwesi, aliishukru serikali kwa kuona umuhimu wa kujenga daraja hilo na kwamba takribani miezi minne tangu mawasiliano ya kata hizo mbili yakatike kumekuwa na changamoto sana kwa wananchi wanapotaka kusafiri kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI