NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Taifa na Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM, Mohammed Ally Kawaida amesema kuwa, pindi serikali itakaporudisha mikopo ya Vijana ambayo ni asilimia nne ya mapato ya ndani Umoja huo hautakuwa tayari kuisikia halmashauri yoyote haina fedha za mikopo hiyo kwani fedha hizo kwa sasa zimekusanywa bila kutumika.
Kawaida ametoa kauli hiyo alipohutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Kimochi wilayani Moshi ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Kamati ya utekelezaji mkoani Kilimanjaro.
Aliwataka vijana kuwa wavumilivu kipindi hiki ambacho serikali imesitisha mikopo hiyo ili kuweka utaratibu mzuri na pindi itakapoanza kutolewa vijana kuchangamkia fursa hiyo.
“kwa sasa mikopo imesitishwa ili kuweka utaratibu vizuri niwaombe vijana tuwe wavumilivu tuendelee kuvuta subira mpaka pale Serikali itakapoturejeshea mikopo yetu” alisema Kawaida.
Mjumbe huyo wa Kamati kuu aliwataka vijana pindi muda utakapofika vijana kutoacha kukopa na badala yake kuunda vikundi kwa wingi ili kunufaika na mikopo hiyo ya Serikali isiyo na riba.
Kawaida alitumia nafasi hiyo kuzionya Halmashauri zote nchi pindi mikopo hiyo itakapofunguliwa isitokee hata moja na kusema haina fedha za kuwakopesha vijana kwani ni kwa muda mrefu sasa mikopo hiyo haijatolewa tangu bajeti ya 2022/23.
“Tunachoamini sisi umoja wa vijana fedha za kuwakopesha vijana zimeendelea kutengwa na kuwekwa sasa ukifika wakati Serikali imefungua mikopo hiyo isitokee halmashauri ikasema haina hela hatutaielewa hata kidogo” alisema Kawaida.
Mwenyekiti huyo aliendelea kudai kuwa, kama ipo halmashauri ambayo imetumia fedha za mikopo ya vijana katika shughuli nyingine waanze kuzitafuta mapema kwani vijana wanahitaji mikopo kwa ajali ya kuboresha maisha yao.
Aidha Mwenyekiti huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwataka vijana kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika kipindi hiki cha uchaguzi wa Serikali za pamoja na uchaguzi mkuu mwakani kwani kila mwanachama anayo haki ya kugombea na kuchaguliwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi alisema kuwa, jimbo hilo limepokea Bilioni 42 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Afya, Elimu, Maji, Barabara na Kilimo.
Prof, Ndakidemi alitumia nafasi hiyo kumuomba Mjumbe wa kamati Kuu huyo, kuwapigania kuhakikisha kata ya Arusha chini nayo inapatiwa skimu ya umwagiliaji ili kuwasaidia wananchi wa kata hiyo kulima kilimo chenye tija na kuondokana na umaskini.
Mwisho.
0 Comments