HATIMAE Kijiji cha Unguja Ukuu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja wametatuliwa changamoto sugu ya kubeba wagonjwa kwa umbali mrefu kwa kupatiwa gari ya kisasa ya kubebea wagonjwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi waliohidiwa na mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said.
Akizungumza katika makabidhiano ya gari hiyo katika kilele cha kuadhimisha miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM hafla iliyofanyika uwanja wa mpira Unguja Ukuu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Mwaka Mrisho Abdalla ameiomba Kamati ya Maendeleo Unguja Ukuu kuhakikisha wanafuata utaratibu wa kutumia gari la kubebea wagonjwa kama ilivyokusudiwa na sio kutumia kinyume na utaratibu.
Amesema, sio jambo jema kwa kamati hiyo kutumia gari hiyo kwa mambo yao binafsi kwani utaratibu unafahamika hivyo ni lazima kufuata sheria za gari kwa kubeba wagonjwa waliozidiwa na kupelekwa katika hospitali kwa haraka ili waweze kupatiwa matibabu.
Aidha amesisistiza kuwa gari hilo ni kwa ajili ya wagonjwa na sio la mtu kwa ajili ya kwenda na shughuli zake binafsi.
"Gari hii Mwakilishi ametoa kwa imani na utekelezaji wa CCM, hivyo ni lazima kuitunza na kuilinda tusije tukasikia mtu anashughuli zake anakodi hili hatutakubaliana nalo hususan chama," alisisitiza.
Naye, Mwakilishi wa Jimbo Tunguu, Simai Mohammed Said, amesema lengo la kutoa gari hiyo ya kubebea wagonjwa ni kutekeleza ahadi yake aliyoitoa kwa kamati hiyo na kusaidia sekta ya afya ambayo inawagusa moja kwa moja wananchi.
Amesema uwepo wa gari hiyo anaamini itaweza kurahisha shughuli za kubeba wagonjwa na kuwafikisha kwa wakati katika hospitali za wilaya, Mkoa au Rufaa na kupatiwa matibabu kwa haraka hasa kinamama wajawazito hatua ambayo itasaidia kuondosha vifo vya mama na mtoto.
Ameahidi kuendelea kusaidia sekta hiyo kwa wadi nyengine ikiwemo Tunguu, Ubago na kila maeneo ambayo yanahitaji kusaidiwa kwa maslahi ya wananchi kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Salum Kibeshi, akizungumza kwa niaba ya jumuiya hiyo amepongeza Mwakilishi Simai kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo na kuhaidi kumuunga mkono katika kuitunza gari hiyo na kutumika kwa lengo lilokusudiwa.
0 Comments