BOT KUANZA KUTUMIA MFUMO MPYA
NA THABIT MADAI,ZANZIBAR BENKI kuu ya Tanzania (BOT), imeanza kutumia mfumo mpya wa uandaaji na utekelezaji wa sera ya fedha ili kuendana na wakati uliopo wa sayansi na teknologia.Naibu Gavana wa Sera za Uchumi na Fedha Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T) Dk. Yamungu Kayandabila, alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa vyombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania katika Ofisi za BOT Zanzibar Kinazini.Alisema taasisi hiyo imeamuwa kuacha kutumia mfumo wa zamani kutokana na kuwa na ufanisi mdogo wa masuala ya huduma za kifedha kulingana na wakati uliopo hivyo mpya unalenga kuleta ufanisi zaidi katika kutekeleza sera ya fedha nchini Tanzania.Akitaja majukumu makuu ya benki hiyo Naibu Yamungu alisema kama zilivyo Benki Kuu zote duniani kazi kuu za BOT ni kusimamia sera ya fedha, kudhibiti mfumuko wa bei na ndio chombo pekee cha kitaifa kilichopewa Mamlaka ya kuchapisha fedha za Tanzania na kusimamia taasisi zote za kifedha nchini Tanzania ikiwemo benki ili kuhakikisha Uchumi endelevu na kulinda haki za wateja wa maiamala ya kifedha.Mbali na hayo alibainisha kuwa BOT ni benki ya serikali, kutoa ushauri juu ya masuala ya Uchumi na Fedha kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Akizungumzia sera ya fedha na sera ya bajeti, alisema ni shilingi moja yenye pande mbili hivyo ni lazima kupitia katika maeneo yote hayo ili kujenga uelewa jinsi sera mbili zinazofanana.Akizungunzia sheria za huduma ndogo za fedha uliyopitishwa mwaka 2018 alisema BOT imepewa jukumu la kusimamia hilo kwa kuona inaanzisha sera ili kuona inaendelea kusimamia jambo hilo kwa kushirikiana na serikali.Hata hivyo, alisema tayari BOT imeanzisha idara inayosimamia malalamiko ya wateja wa fedha ambapo hapo nyuma kulikuwa hakuna Idara hiyo jambo ambalo ni mageuzi makubwa ndani ya BOT hivyo aliwataka wananchi kutumia Idara hiyo kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kushughulikiwa kwa haraka."Wakati unachukua mkopo benki haikwambii vizuri au husomi vizuri sasa tunaandaa miongozo ambayo itawataka watu wanaotoa mikopo kuweka wazi jambo hilo ili wale wanaokwenda kuchukua mkopo waweze kujua na kufahamu zaidi," alibainisha.Mbali na hayo, alipongeza mashirikiano ya karibu yaliyokuwepo baina ya BOT na vyombo vya habari nchini katika kusaidia kutoa elimu ya benki hiyo juu ya majukumu yake na kuahidi kuendeleza mashirikiano hayo ili kuendelea kufahamu majukumu ya Benki Kuu na kuyafikisha kwa jamii kwani elimu ya fedha ina umuhimu mkubwa kwa wananchi katika maisha yao ya kila siku ili kuepuka utapeli.Naye Kaimu Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Zanzibar, Masoud Suleiman, alisema lengo la Mafunzo hayo ni kupata uelewa wa kazi wanazozifanya benki kuu na imekuwa ni utaratibu wa benki hiyo kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa bahari.Alisema ni mategemeo yake kuwa wanahabari hao watatumia muda wote kujifunza kwa Yale waliyoyaandaa na kuamini watakuwa mabalozi wazuri kwa jamii ya Tanzania kutoa katika kutoa elimu ili waweze kuelimisha jamii.Akiwasilisha mada ya utekelezaji wa sera ya fedha Meneja Msaidizi Uchambuzi wa sera ya fedha, John Mero alisema mafanikio ya kiuchumi yanategemea sera mbalimbali ikiwemo sera hiyo ya fedha, sera za kibajeti na sera ya kisekta ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kufia malengo ya nchi.Aidha alisema sera ya fedha hujumuisha maamuzi na hatua zinachukuliwa na BOT kupunguza, kuongeza ujazi wa fedha ili kufikia malengo ya kiuchumi.Akizungumzia malengo ya sera hiyo alisema ni kuhakikisha kiwango cha fedha kilichokuwepo kwenye Uchumi kinakudhi mahitaji ya uchumi, kiwango kikubwa cha fedha katika mzunguko zaidi ya mahitaji ya shughuli za Uchumi hupelekea kuongezeka kwa bei za bidhaa hivyo utekelezaji wa sera hiyo unalenga utulivu wa bei za bidhaa na huduma na kuwezesha shughuli za kiuchumi.Naye Meneja Msaidizi Utafiti BOT Lusajo Mwamkemwa, alisema malengo ya sera ya fedha ni kudhibiti mfumuko wa bei (kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma), kuvutia uwekezaji, uzalishaji, biashara, kulinda uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha.Alisema sera ya fedha ina mchango mkubwa katika maendeleo ya ukuaji wa uchumi wa nchi.Akizungumza kwa niaba ya wandishi wa habari Mwenyekiti wa Mafunzo hayo Salma Said aliipongeza BOT kuandaa Mafunzo hayo ambayo yatasaidia vyombo vya habari kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya fedha yanayosimamiwa na benki kuu ya Tanzania nchini.Katika mkutano huo mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwemo maendeleo ya utekelezaji wa sheria ya huduma ndogo za fedha,mikopo, faida na athari zake isiposimamiwa vizuri, ustawi, ujumuishi wa huduma za fedha na kulinda mtumiaji wa huduma za fedha na faida za kutumia njia mbadala za malipo badala ya pesa taslim.
0 Comments